MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imekiri kuziandika
waraka kampuni za simu nchini kuzitaka zianze kukata kodi mpya ya laini mara
moja kuanzia mwezi huu. Kodi hiyo mpya ilipitishwa wakati wa Bunge la Bajeti ya
mwaka wa fedha 2013/2014 na kutaka utekelezaji wake uanze Julai 30, ili
kusaidia shughuli za bajeti ya Serikali Kuu.
Akijibu swali kuhusu ukweli wa Mamlaka hiyo kuagiza
kampuni hizo kuanza rasmi kutoza kodi hiyo mwezi jana, Mkurugenzi wa Elimu kwa
Mteja, Huduma na Mapato wa TRA, Richard Kayombo, alikiri kutoa agizo hilo.
“Sitaki kuzungumzia kiundani sana suala hili, lakini
ukweli ni kwamba kampuni hizi za simu zimeandikiwa kuanza kulipa kodi na
tumeandika kwa ajili ya utekelezaji wa kodi hii mpya,” alisema Kayombo.
Alisema ingawa kweli kampuni hizo zimeagizwa kuanza
kutoza kodi hiyo, hatazungumzia zaidi suala hilo kwa kuwa tayari liko
mahakamani, hivyo si vema kuingilia uhuru wa mhimili huo. Wakati TRA ikitoa
agizo hizo, Taasisi ya Watumiaji wa Bidhaa na Huduma ilifungua kesi Mahakama
Kuu kupinga sheria hiyo.
Taasisi hiyo ilifungua kesi hiyo hivi karibuni katika
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya dharura na kuanza
kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu ambao ni Lawrence Kaduri, Aloysius
Mujulizi na Salvatory Bongole.
Msingi wa kesi hiyo unaosimamiwa na mawakili wa upande
wa ulalamikaji wa Rex ni kuiomba Mahakama hiyo itangaze kuwa sehria
iliyopitishwa na Bunge ya kila mtumiaji wa simu ya mkononi kukatwa Sh 1,000 kwa
mwezi ni kandamizi.
Aidha, wanataka Mahakama hiyo imzuie Waziri wa Fedha
kupitia TRA kutoza kodi hiyo hadi maombi yao yatakapotolewa uamuzi. Pamoja na
TRA kukiri kutoa agizo la kuanza kukatwa kwa kodi hiyo na kutofafanua, kuna
taarifa zilizoandikwa na gazeti moja la kila siku kuwa waraka huo umezitaka
kampuni hizo kuanza kutoza kodi hiyo ya Julai, Agosti na Septemba na kuendelea.
Tangu kupitishwa kwa kodi hiyo na Bunge, Aprili mwaka
huu, kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, wanasiasa na
wanaharakati ya kuipinga kwa kuwa itafanya wananchi wengi wenye kipato kidogo
kushindwa kumudu gharama za kumiliki simu.
Malalamiko hayo yalimlazimu Rais Jakaya Kikwete kukutana
na wadau wa mawasiliano ambao ni wamiliki wa Kampuni za Simu Tanzania (MOAT),
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na teknolojia, January Makamba na Waziri
wa Fedha, William Mgimwa, kasha kuwaagiza wakae na kufikiria mbadala wa kodi
hiyo kama itaondolewa, jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.
Kampuni hizo za simu zikitekeleza agizo la waraka huo
mwezi jana, takriban wateja milioni nane wa simu watakatwa Sh 3,000 ili kufidia
kodi ya simu ya Sh 1,000 kwa kila mwezi kuanzia Julai kodi hiyo ilipotakiwa
kuanza kutozwa kisheria kwa kila mtumiaji wa simu.
CHANZO: Habari Leo
0 comments:
Post a Comment