Samantha Lewthwaite, the ‘Mjane Mweupe’ anayesakwa kwa
kushukiwa kuongoza shambulizi la Nairobi, ni mke au alikuwa ameolewa kwa siri
na afisa wa zamani wa Jeshi la Wanamaji la Kenya, gazeti moja limenukuu taarifa
za siri kutoka Polisi ya Uingereza, Scotland Yard.
Mumewe mpya ni Bwana Abdi Wahid, ambaye gazeti hilo
limesema kuwa kwa sasa yupo Ulaya.
Hata hivyo, Inspekta Jenerali David Kimaiyo anasema kuwa
hawakuwa wakijua kwamba “Mjane Mweupe” alikuwa ameolewa na askari wa zamani wa
jeshi la Kenya.
“Hivi sasa ndiyo ninalisikia hili. Tunachojua ni kwamba
alikuwa akiishi ni mtu mjini Mombasa ambaye alishtakiwa mahakamani na hivyo
hatumjui mtu mwingine anayehusika,” alisema Bw. Kimaiyo said.
Mumewe wa kwanza, Jermaine Lindsay, alijilipua katika
shambulizi la kujitoa mhanga nchini Uingereza mwaka 2005.
Alikuja Afrika mwaka 2009 na amekuwa akizunguka na
kuishi barani huku kwa zaidi ya miaka 2.
Taarifa hizi zimeibuka wakati Wabunge wakiahidi kutumia
mamlaka yao kuubadilisha kabisa mfumo wa usalama, ikiwa ni pamoja na kuzifunga
kambi za wakimbizi na kuwaondoa wakuu wa usalama wenye utendaji mbovu.
Wakati kamati mbili za ulinzi na usalama zikianza
kuwahoji wakuu wa usalama leo, waliahidi kwenda kwenye kiini cha shambulizi la
Westgate, ikiwemo kuchungumza utendaji wa idara za usalama zinazochunguza tukio
hilo katika wakati ambapo kuna madai ya wizi uliofanywa na wanausalama kwenye jingo
hilo.
“Tunataka kujua ukweli kuhusu kilichotokea Westgate,
ikiwa ni pamoja na kujua historia, wahusika na kilichosababisha kushindwa
kulidhibiti tukio hilo,” alisema mwenye kiti wa kamati ya ulinzi na uhusiano wa
kimataifa, Ndung’u Gethenji.
Wahid alikamatwa mwaka 2011 baada ya polisi kubaini kuwa
nyumba yake ya mjini Mombasa ilikuwa imegeuzwa kuwa kiwanda cha kutengenezea
mabomu kikiendeshwa na Lewthwaite na washirika. Hakupelekwa mahakamani.
Awali alikuwa akitambuliwa kama mtu aliyepangisha nyumba
aliyokuwa akiishi Lewthwaite, lakini haikuwa ikifahamika wazi ni kwa kiasi gani
alikuwa na taarifa za vitendo vya kigaidi vilivyokuwa vikifanywa na mkewe.
Lakini jana, Al-Shabaab ilisisitiza kuwa hakuna mwanamke
aliyeshirikiana nao katika shambulio la Nairobi, na kukanusha taarifa kuwa “Mjane
Mweupe’ alishiriki katika mauaji hayo.
“Kwa mara nyingine tunatangaza wazi kuwa hakuna mwanamke
aliyehusika na tukio la Westgate,” walisema Al-Shabaab kwenye akaunti yao ya Twitter,
wakisisitiza juu ya sera yao ya “kutowatumia wanawake katika operesheni kama
hizo”.
Wakati huo huo, ripoti kutoka Somalia zinasema kuwa jana
kiongozi mmoja wa dini ya Kiislamu katika mji wa Hargeisa alikamatwa kuhusiana
na shambulizi la Westgate.
Mohamoud Abdullahi Ghelle alikamatwa kwa madai ya kuunga
mkono shambulizi hilo lililogharimu maisha ya watu 67 na kuwajeruhi zaidi ya
175.
Inasemekana kuwa uhusiano wa Wahid na Lewthwaite “umewapa
tabu wapelelezi, hasa ikizingatiwa kuwa aliwahi kuwa mwanajeshi na aliwahi
kufanya kazi kama afisa usalama nchini Afghanistan, akiwalinda wamagharibi
dhidi ya mashambulizi ya Wataleban”.
Mapema jana Jumatatu, Shirika la Msalaba mwekundu nchini
Kenya lilitangaza kuwa idadi ya watu waliopotea baada ya shambulio la Westgate
imeshuka mpaka 39 kutoka ile ya awali ya watu 60.
Katibu Mkuu wa shirika hilo, Abbas Gullet, alisema kuwa
watu 14 kati ya wale waliokuwa wameripotiwa kupotea walikutwa wakiwa hai na
kuruhusiwa kutoka hospitali mbalimbali, huku watu saba wakithibitika kufariki
dunia.
CHANZO: DAILY NATION
0 comments:
Post a Comment