MAREKANI imechukua hatua ya kuzuia misaada ya kijeshi
kwa nchi tano, zikiwemo tatu za Kiafrika, kwa tuhuma za kutumia watoto kama
askari katika vita mbalimbali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya
nje ya nchi hiyo, vikwazo hivyo vinaiathiri Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda
na Sudan kwa upande wa Afrika, huku nchi nyingine zikiwa ni Myanmar na Syria.
"Lengo letu ni kufanya kazi na nchi
zilizoorodheshwa ili kuhakikisha kwamba uhusishaji wowote wa askari watoto –
utoaji wa mafunzo ya kijeshi kwa watoto – unakomeshwa,” alisema Naibu waziri wa
mashauri ya kigeni wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Linda
Thomas-Greenfield.
Nchi nyingine tatu ambazo majeshi yake yanajulikana
kuwapa watoto mafunzo ya kijeshi, lakini zimesamehewa ni pamoja na Chad, Sudan
Kusini na Yemen, anasema afisa mmoja wa Wizara hiyo ambaye hakutaka kutajwa
jina lake.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia zimesamehewa
kiasi, alisema afisa huyo na kuongeza kuwa utawala wa Obama umeamua kuzisamehe
nchi hizo “kwa maslahi ya Marekani.”
Kwa sheria, Wizara ya Mashauri ya Nje ya Marekani
inalazimika kuzifuatilia nchi ambazo serikali azake zinawapa mafunzo na
kuwatumia watoto kama askari katika ripoti yake ya kila mwaka juu ya biashara
ya binadamu. Nchi kumi zilizoathiriwa na hatua ya leo zote zilikuwa
zimeorodheshwa katika uchunguzi mpya kabisa wa wizara hiyo, iliyotolewa mwezi
Juni.
Nchi hizo zinaweza kunyimwa aina Fulani ya misaada ya
kijeshi kutoka Marekani isipokuwa kama Ikulu ya nchi hiyo itaamua kuzisamehe. Sheria
hiyo iliyotungwa mwaka 2008 pia inawaruhusu maafisa wa Marekani kuzuia leseni
za mataifa hayo yanapotaka kununua zana za kijeshi.
Hata hivyo haijawa wazi ni kwa kiasi gani misaada hiyo
itazuiliwa kutokana na hatua iliyochukuliwa leo.
Rwanda haikupewa msamaha kwa sababu ya kuhusika kuwaunga
mkono waasi wa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, alisema Thomas-Greenfield,
mwanadiplomasia wa juu wa Marekani kwa Afrika, kwenye mahojiano ya mtandaoni na
wanahabari yaliyotangazwa kwenye tovuti ya Wizara ya Mambo ya Nje.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa pamoja na Serikali ya
Kongo wanatuhumu Rwanda kwa kuwafadhili waasi, madai yanayokanushwa na Rwanda.
"Msaada wowote unaotolewa kwa makundi hayo ya waasi
unachukuliwa kama ni kufadhili mapigano katika eneo zima,” Thomas-Greenfield aliwaambia
wanahabari na kuongeza kuwa maafisa wa Marekani wataendelea kujadili suala hilo
na serikali ya Rwanda.
Marekani itaendelea kuunga mkono juhudi za kulinda amani
nchini Rwanda, alisema afisa huyo.
CHANZO: TodayZaman
0 comments:
Post a Comment