WAZIRI Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, amelaani
vikali shambuli la kigaidi lililofanywa hivi karibuni na kundi la al-Shabaab
lenye mafungamano na al-Qaeda kwenye kituo cha kibiashara mjini Nairobi, akisema
kuwa Uislamu hauruhusu kuua raia wasiokuwa na hatia.
Akizungumza jana katika mkoa wa Denizli, magharibi mwa
Uturuki, alisema: “Wanadai kuwa wanafanya hivi kwa jina la Uislamu. Sikilizeni:
Mwenyezi Mungu hajampa mtu mamlaka ya kuwaua watu wasiokuwa na silaha wala
ulinzi. Kumuua mtu mmoja ni sawa na kuwaua watu wote. Hivi ndivyo dini yetu
inavyosema.”
Katika shambulizi la wiki iliyopita kwenye jengo la
biashara la Westgate mwanamke mmoja wa Kituruki, Elif Yavuz, aliuawa. Mwanamke huyo
kutoka Chuo Kikuu cha Harvard alikuwa akitarajia kujifungua ndani ya wiki
mbili. Mume wake, mhandisi mwenye uraia wa Australia, Ross Langdon, naye pia
aliuawa katika shambulizi hilo.
Aidha, Erdoğan alilaani vikali shambulizi lililofanywa wiki
iliyopita kwenye kanisa moja mjini Peshawar, nchini Pakistan na kuua waumini
85.
“Tunalaani vitendo vyote vya kinyama vinavyofanywa Iraq,
Yemen, Lebanon na Syria. Ugaidi hauna dini, na kamwe hatuwezi kukubali neno ‘Uislamu’
na ‘Ugaidi’ kuwekwa pamoja… Wale wanaojaribu kuyaweka pamoja maneno haya ili
kutengeneza chuki dhidi ya Uislamu ni wabaguzi. Wale wanaotofautisha kati ya
magaidi wazuri na magaidi wabaya ni wahalifu na ndio wanaolea ugaidi.”
Makundi ya Al-Shabaab na al-Qaeda yalitangaza kuungana
mwezi Februari 2012.
CHANZO: TodayZaman
0 comments:
Post a Comment