MKAZI wa Kijiji cha Mlongazila, wilayani Kisarawe,
Pwani, Moshi Hamad anatuhumiwa kumng’ata mwanaye, Khadija Hamad (6) sehemu za
siri kwa madai ya kujisaidia haja kubwa na ndogo hovyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima juzi
wilayani Kisarawe, wakazi hao walisema mama huyo amekuwa na tabia ya kumfungia
ndani mtoto wake huyo na kumchapa kwa zaidi ya nusu saa, akitumia nyaya za simu
na kumng’ata sehemu mbalimbali za mwili zikiwamo za siri na kumsababishia
maumivu makali.
Wakazi hao walisema waliamua kutoa taarifa kwenye dawati
la haki za binadamu baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo, na sasa wamelitaka
Jeshi la Polisi kumkamata mama huyo na kumchukulia hatua.
Stella Musa, alisema sehemu za siri za mtoto huyo
zimeharibiwa kutokana na kung’atwa na meno, huku zikiwa na vidonda vinavyodaiwa
vimetokana na kuchomwa na kitu chenye ncha kali.
“Wazazi wa mtoto huyo ni wanangu, siku moja mama huyo
alimuumiza mkono. Nilimchukua na kukaa naye nyumbani kwangu kwa mwezi mmoja
nikimuhudumia kwa kumkanda kwa maji ya moto,” alisema Stella.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Mlongazila, Paulo Idana
ambaye pia ni katibu wa dawati la kutetea haki za binadamu, alisema suala hilo
limewafikia, hivyo wanachukua hatua za kisheria huku mtoto huyo amewekwa chini
yao kwa matibabu zaidi.
“Tulimfuata mama huyo Septemba 20 mwaka huu na tulifanya
nae mahojiano mbele ya ofisa mtendaji wa kijiji na alikiri akisema alifanya
hivyo kwa sababu ya hasira. Tunafanya utaratibu ili tumfikishe kwenye vyombo
vya sheria,” alisema Idana.
Akieleza mkasa huo, mtoto huyo alisema wakati mwingine
mama yake alikuwa akimwita ili amfundishe kusoma na aliposhindwa aling’atwa
mgongoni, mapajani na sehemu za siri huku akisema atamfanyia hivyo hadi ajue
kusoma.
Mama wa mtoto huyo, Moshi, alisema alikuwa akitoa adhabu
kwa mwanaye huyo kutokana na kujisaidia haja ndogo na kubwa hovyo wakati
akirudi shule.
“Nafanya hivi kutokana na hasira siwezi nikamuona mtoto
wangu anajisaidia haja kubwa na ndogo kwenye nguo nikamwacha tu, lazima
nimwadhibu… jana alitapika kwenye sahani. Je, mtoto kama huyu nitamwacha?”
alihoji Moshi.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Khadija Samizi alikiri
kuwepo kwa tukio hilo.
0 comments:
Post a Comment