Rais wa Iran, Hassan Rouhani (kulia) na Rais Barack Obama wa Marekani (kushoto) |
RAIS wa Iran
bwana Hassan Rouhani na mwenzake wa Marekani bwana Barack Obama wamefanya
mazungumzo kwa njia ya simu wakati rais wa Iran akikamilisha ziara yake kwenye
hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Shirika la habari la Iran, IRNA, limeripota kuwa Rouhani
alipokea simu kutoka kwa Rais Obama leo Ijumaa wakati akielekea uwanja wa ndege
wa kimataifa wa John F. Kennedy kwa safari ya kurejea Tehran.
Viongozi hao walisisitiza juu ya utashi wa kisiasa wa nchi
zao kutafuta muafaka juu ya programu ya
nyuklia ya Iran, na walibadilishana mawazo kuhusu mambo kadhaa, ikiwemo
ushirikiano katika mambo mbalimbali ya kieneo.
Aidha, wakati wa mazungumzo hao, waliwapa Mawaziri wa
Mashauri ya Kigeni wa nchi hizo, bwana Mohammad Javad Zarif wa Iran na bwana John
Kerry wa Marekani, jukumu la kuandaa uwanja kwa ajili ya ushirikiano baina ya
mataifa hayo mawili.
Mazungumzo hayo ya simu ni ya kwanza baina ya marais wa
nchi hizo mbili tangu mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979, na yamefanyika kufuatia
kikao cha jana Alhamisi baina ya Iran na mataifa sita yenye nguvu uliofanyika
mjini New York kuhusu programu ya nyuklia ya Iran.
Kerry aliyaita mazungumzo hayo kuwa “yenye kujenga,”
akisema, “tumekubaliana kufanya juhudi ya kuendelea na mchakato utakaotengeneza
msingi na kutafuta njia ya kupata majibu ya maswali ambayo watu wanayo kuhusu
programu ya Nyuklia ya Iran.”
Naye waziri wa mashauri ya kigeni wa Iran, Muhammad Zarif,
aliyasifu mazungumzo hayo kama “mazuri sana na yenye mafanikio” na kusema kuwa
matokeo ya mazungumzo hayo yalijumuisha suala la “kuondosha kabisa” vikwazo
vyote dhidi ya Iran.
“Tunatumai tutaweza kupiga hatua kulitafutia ufumbuzi
suala hili na kuhakikisha kuwa hakuna wasiwasi juu ya program ya Iran ambayo ni
ya amani,” alisema bwana Zarif.
Iran imekuwa ikituhumiwa na mataifa ya Magharibi na
wataifaki wao kuwa programu yake ya nishati ya nyuklia inalenga kutengeneza
silaha za maangamizi.
Hata hivyo, Iran imekuwa ikikanusha tuhuma hizo na
kusema kuwa mradi wake huo ni kwa ajili ya malengo ya amani.
CHANZO: Press Tv
0 comments:
Post a Comment