![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEhXMUEOnsJdg-0y_Me9sOJvU2r4rnKYRshJguy_-Akbop6dhspKzlj8hyphenhyphenldoO50G8H3aroGJ561fSvW0DgHuzCeO_g0JsHuAZqrrmxePHavRD7-iT38ZfwnA7ELtRwvADndEDH-R-kmRys/s1600/various-sim-cards.jpg)
ZIKIWA zimebakia siku mbili kabla ya serikali kuanza
kuwatoza kodi ya laini (sim card) watumiaji wa simu, Taasisi ya Watumiaji wa
Bidhaa na Huduma imefungua kesi Mahakama Kuu kupinga sheria hiyo.
Taasisi hiyo ya Consumers of Goods and Services Across
the Country ilifungua kesi hiyo juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini
ya hati ya dharura na kuanza kusikilizwa jana mbele ya jopo la majaji watatu.
Majaji waliosikiliza kesi hiyo ni Lawrence Kaduri,
Aloysius Mujuluzi na Salvatory Bongole.
Katika kesi hiyo walalamikaji wanaiomba mahakama
itangaze kwamba sheria iliyopitishwa na Bunge inayotaka kila mtumiaji wa simu
ya mkononi kukatwa sh 1,000 kila mwezi ni kandamizi.
Walidai kwamba watumiaji wengi wa simu za mkononi hawana
uwezo wa kukatwa fedha hiyo kwa mwezi, huku wakisisitiza kuwa itawaathiri
watumiaji wa huduma hiyo.
Kwa mujibu wa madai ya walalamikaji hao, sheria hiyo
inakiuka matakwa ya katiba ya nchi ya uhuru wa kupashana habari na kuiomba
mahakama kuifuta sheria hiyo waliyoiita kuwa kandamizi.
Mawakili wa walalamikaji kutoka Kampuni ya uwakili ya
Rex, Lugano Mwandamo na Merkizedeki Lutema walidai kuwa wateja wao wanataka
mahakama imzuie Waziri wa Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) kutoza kodi
hiyo hadi hapo maombi yao yatakapotolewa uamuzi.
“Kuanzia sasa hivi mahakama itoe amri ya muda kuzuia
utekelezaji wa sheria hiyo usitendeke,” alidai Mwandamo.
Kutokana na maombi hayo, jopo la majaji liliahirisha
kesi hiyo hadi Oktoba 3 mwaka huu, likimtaka wakili wa serikali, Kelley Mwitasi
kuwasilisha maelezo yake kwa njia ya maandishi.
Wakati huo huo, majaji hao waliutaka upande wa
walalamikaji kujibu maelezo ya upande wa serikali kwa njia ya maandishi na
kuyawasilisha mahakamani hapo kabla ya Oktoba 7, ambapo kesi hiyo itaanza
kusikilizwa saa saba mchana siku hiyo.
Kufunguliwa kwa kesi hiyo kutasitisha utekelezaji wa
utozaji wa kodi hiyo unaotakiwa kuanza Septemba 30 mwaka huu, baada ya TRA
kuziandikia kampuni za simu waraka wa kuzitaka zianze utekelezaji wa sheria
hiyo.
Sheria hiyo iliyopingwa na wanasiasa wengi bila kujali
itikadi za vyama vyao, ilipitishwa kwa nguvu ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) wakati wa Bunge la Bajeti na kutaka utekelezaji wake uanze Julai 30.
Bunge kupitia Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa
Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM) lilitaka kuwapo kwa kodi hiyo ili
kusaidia shughuli za bajeti ya serikali kuu.
Kupitishwa kwa kodi hiyo kuliibua malalamiko ya
wanasiasa hata wa CCM dhidi ya Chenge anayelazimisha kuwapo kwa kodi hiyo, huku
akishindwa kuamini kwamba kuna Mtanzania anayekosa sh 1,000 kwa mwezi kwa ajili
ya laini ya simu.
Malalamiko hayo, yalimlazimu Rais Jakaya Kikwete
kukutana na wadau wa mawasiliano ambao ni wamiliki wa kampuni za simu Tanzania
(MOAT), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na
Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kisha kuwaagiza waiondoe kodi hiyo.
“Nakuombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja,
wekeni akili yenu pamoja tutafute namna gani tutajaza pengo hili la sh bilioni
178 endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na
kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,” alisema rais kwenye kikao
hicho.
Licha ya agizo la rais kutekelezwa kwa MOAT kutakiwa
kuongeza kodi nyingine iitwayo ‘Excise duty’ kutoka asilimia 14 hadi 17 bila
kujali kwamba katika Bunge la bajeti kodi hiyo iliongezwa kutoka asilimia 12
hadi asilimia 14, kodi ya laini za simu haijaondolewa.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na mawasiliano walisema
kutojadiliwa kwa mabadiliko ya kodi hiyo ya simu ni dalili kwamba Waziri wa
Fedha amezidiwa nguvu na kiti cha spika kinachounga mkono hoja hiyo ya Chenge
na kushindwa kutekeleza agizo la rais.
Takwimu zilizotolewa na kampuni za simu zinaonyesha kuwa
miongoni mwa wamiliki wa laini za simu milioni 22; milioni nane wanatumia chini
ya sh 1,000 kwa mwezi.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment