HATIMAYE mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngasa, amelipa
faini ya sh milioni 45 kama alivyokuwa ameadhibiwa na Kamati ya Sheria na Hadhi
za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kuwekewa pingamizi
la usajili ya klabu ya Simba.
Simba ilipinga Ngasa kusajiliwa na Yanga kwa madai ina
mkataba naye walioingia wakati wakimsajili kwa mkopo kutoka Azam FC msimu
uliopita, ambapo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti
wake, Alex Mgongolwa, ilimhukumu mchezaji huyo kutocheza mechi sita na kulipa
sh milioni 30 alizokuwa amechukua kwa Wekundu wa Msimbazi na riba asilimia 50,
ndipo aweze kurejea dimbani.
Kutokana na kulipa fedha hizo, Ngasa anatarajiwa kushuka
dimbani leo kuwavaa Ruvu Shooting katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Uwanja wa
Taifa jijini Dar es Salaam.
Majira ya saa 9 alasiri jana, Ngasa aliwasili makao
makuu ya TFF Karume Ilala, akiwa amebeba begi jeusi lenye hundi ya fedha hizo,
akisindikizwa na watu watatu akiwemo mjumbe wa sekretarieti ya Yanga, Mkenya
Patrick Naggi.
Mara baada ya kukabidhi hundi hiyo katika ofisi ya fedha
ya shirikisho hilo, Ngasa alisema ameamua kulipa fedha hizo ili aweze
kuitumikia klabu yake ya Yanga katika mchezo wa leo, kwani anaumizwa na matokeo
ambayo timu yake inayavuna kwa sasa.
Aidha Ngasa aliwataka wachezaji wenzake kutofanya ambayo
yeye kayafanya na kuwashauri kutafuta wanasheria ambao watakuwa wakisimamia
haki zao.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile
Osiah, alisema jana kuwa kuanzia msimu huu kila mchezaji mwenye mkataba na
klabu yake, ametengenezewa leseni ambayo itakuwa ikionyesha kuanza kwa mkataba
na kumalizika kwake.
Osiah alisema wameamua kufanya hivyo baada ya kuona hodi
zinazidi TFF kwa wachezaji kuulizia mikataba yao na kusababisha usumbufu usio
wa lazima, hivyo kwa utaratibu huo watakuwa wamefanikiwa kuuepusha.
Akizungumzia mchezo wa leo, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie
Brandts, alisema kuwa yuko tayari kumtumia mchezaji huyo kwa kuwa ni kati ya
anaowahitaji katika kikosi chake na alitamani kufanya hivyo siku zilizopita ila
ilishindikana kutokana na adhabu hiyo.
Brandts alisema mchezo wa leo ana imani kubwa timu yake
itaibuka na ushindi, kutokana na marekebisho aliyoyafanya mara baada ya
kukubali kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Azam FC Jumamosi iliyopita.
Mbali na mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani
mkubwa, mechi nyingine ni kati ya Rhino Rangers na Kagera Sugar dimba la Ali
Hassan Mwinyi Tabora huku Mbeya City wakiwakaribisha Coastal Union uwanja wa
Sokoine na Mgambo JKT watakuwa wenyeji wa ndugu zao JKT Oljoro kwenye uwanja wa
Mkwakwani Tanga.
0 comments:
Post a Comment