MAKACHERO wa kimataifa kwa kushirikiana na wale wa
Kenya, wamesema kuwa wamepata gari wanaloamini lilitumiwa na kundi la kigaidi
la Al-Shabaab wakati walipofanya shambulizi katika jengo la kibiashara la
Westgate jijini hapa na kuua watu zaidi ya 67.
Taarifa hizo zimetolewa na mmoja wa maofisa ambaye
hakupenda kutaja jina lake kwa sababu ya kutovuruga uchunguzi wao, akisema kuwa
njia wanayotumia ni kufuatilia wamiliki wa magari wanayoyakuta nje ya jengo
hilo.
Aliongeza kuwa kwa sasa bado wanaendelea kuyatazama
magari mengine ambayo yapo nje ili kuyagundua zaidi yalivyotumiwa na
washambuliaji.
Katika taarifa nyingine zilizotolewa na Muungano wa
Waandishi wa Habari, zimeeleza kuwa wanahabari wao waliwashuhudia makundi ya
wachunguzi wa Kenya na wale wa kigeni wakiwa wanalichunguza gari hilo aina ya
Saloon lenye rangi ya fedha, lililokuwa imeegeshwa mita 20 kutoka kwenye lango
la kuingilia kwenye jengo hilo.
Walisema kuwa gari hilo lilikuwa limefunguliwa mlango wake,
huku wachunguzi hao wakiwa wanalipiga picha ikiwa ni pamoja na kuandika, lakini
waligoma kuzungumzia kile walichokiona.
Polisi wa nchini Kenya wamekuwa hawatoi taarifa kwa kina
tangu washambuliaji hao walipotoa vitisho kwa mataifa ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Waziri wa Usalama wa Ndani, Joseph ole
Lenku, uchunguzi huu utachukua muda wa wiki moja kuhakikisha wanaopoa miili ya
watu ambao wamefukiwa kwenye jengo hilo kama wapo.
Kundi la Al-Qaeda linalofungamana na Al-Shabaab limetoa
vitisho vya kuwepo kwa shambulio jingine kutokana na Serikali ya Kenya kupeleka
vikosi vyake kuishambulia Al-Shabaab nchini Somalia.
Kazi ya kutafuta wahalifu wa tukio hilo inafanywa na
mawakala wa FBI kutoka Marekani, vikosi vya usalama vya Uingereza, Canada na
Ujerumani.
Pamoja na uchunguzi huo, pia taarifa kutoka ndani ya
Jeshi la Kenya zimeeleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa washambuliaji wa tukio
hilo kukimbia siku waliyokuwa wamefanya tukio hilo.
Kikosi cha Msalaba Mwekundu kinasema kuwa watu 61
hawajulikani waliko.
Lakini idadi ya watu waliofariki imebaki kuwa
kitendawili kutokana na serikali kusema ni 67 huku vikosi vya Al-Shabaab
vikisema ni zaidi ya 177.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Kenya imesema kuwa
shambulio la kigaidi halijaathiri mipango yake ya kuongeza karibu dola bilioni
1.5 kwenye makubaliano yao ya ubia wa kimataifa.
Kenya inatafuta nafasi kubwa katika masoko ya kimataifa
ili kufufua miundombinu ya tangu kipindi cha ukoloni ambayo kwa sasa
imeharibika na kuongeza kasi ya uchumi ambao umeporomoka.
Mpango huo wa ubia wa kimataifa ambao utakuwa wa kwanza
mkubwa katika taifa hilo la ukanda wa jangwa la Sahara, umepangwa kufanyika
baadaye Novemba mwaka huu.
Katibu wa Hazina, Henry Rotich alisema kuwa uchumi wa
Kenya kama ilivyo ari ya watu wake, haujatikiswa na janga hilo la hivi
karibuni.
0 comments:
Post a Comment