Vurugu kubwa jana ziliibuka wilayani Hai Kilimanjaro na
kulilazimu Jeshi la Polisi kufyatua mabomu ya machozi katika jitihada za kuzima
vurugu hizo.
Hata hivyo, hali iliendelea kuwa tete ilipofika saa
10:00 alasiri na kulazimu Jeshi la Polisi kuongeza nguvu kwa kuwatuma askari
zaidi wa kutuliza ghasia (FFU) kutoka Moshi Mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha
kuibuka kwa vurugu hizo zilizoanza saa 6:00 mchana katika Kijiji cha Kwansera
huko Masama.
“Ni kweli kuna vurugu kati ya Wananchi wa hicho kijiji
na mwekezaji anayemiliki shamba kubwa la kahawa na migomba ndiyo vijana wetu wa
FFU wameelekea huko,” alisema.
Taarifa zaidi kutoka eneo la tukio zilisema Polisi wenye
sare kutoka Kituo cha Bomang’ombe wilayani Hai ndio wa kwanza kufika eneo la
tukio na kujaribu kudhibiti vurugu bila mafanikio.
“Mabomu ya kutosha yameshafyatuliwa hapa tangu saa 6:00
mchana, lakini hali siyo nzuri wananchi wanataka kuchoma moto majengo ya
mwekezaji,” kilidokeza chanzo chetu.
Kiini cha mgogoro huo ni uhasama uliojengeka kati ya
wananchi hao na mwekezaji huyo Mtanzania kutokana na mwekezaji kuhodhi eneo
kubwa huku wananchi wakiwa hawana ardhi.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment