Idadi ya wanawake wanaoota ndevu mithili ya wanaume
inazidi kuongezeka nchini. Hali hiyo imewashtua pia wataalamu wa afya, ambao
wamesema ingawa hakuna takwimu halisi ya wenye tatizo hilo, lakini hali
inatisha.
Uchunguzi uliofanywa kuhusiana na suala hilo umebaini
kuwa hali hiyo inasababishwa na mambo mbalimbali, yakiwemo ya kurithi, utumiaji
mbaya wa vyakula na matumizi holela ya vipodozi.
Daktari Adam Nyalandu kutoka Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), alisema kuwa tatizo la wanawake tatizo la wanawake kuota ndevu
linatokana na sababu nyingi ikiwemo matumizi ya vipodozi vyenye kemikali na
vyakula vya kusindika.
Alisema matumizi ya vipodozi vya aina tofauti vyenye
viambata vya sumu vimekuwa vikichangia madhara mbalimbali kwa wanawake ikiwemo
uotaji wa ndevu.
Pia alisema baadhi ya wanawake wamekuwa wakitumia
vipodozi vya aina tofauti ili kutakatisha ngozi zao zionekane kama za wazungu
bila kujua madhara yake. Alisema vipodozi vingi vina viambata vyenye sumu
ambayo ni tishio kiafya.
Dk. Nyalandu alifafanua kuwa baadhi ya vyakula vya
kusindika vimekuwa vikitengenezwa kwa kutumia kemikali nyingi ambazo
zinachangia tatizo hilo kwa wanawake, ambapo madhara yake kwao yameanza
kuonekana waziwazi.
“Mfano ulikuwa huli nyama za kopo au vyakula vya
kusindika ambavyo kemikali inatumika kuvisindika sasa unakula, vinaweza
kusababisha hilo tatizo kwa kiwango kikubwa,” alisema Dk. Nyalandu.
Alisema ni vema wanawake wakawa makini na vipodozi
wanavyotumia kwa kuchunguza viambata vya sumu ili kuepuka kuvitumia kwa usalama
wa fanya zao.
Kwa upande wake, Dk. Abdallah Mandai aliwaonya wanawake
na kuwataka kuachana na matumizi ya vipodozi vyenye kemikali sanjari na ulaji
wa vyakula vya kizungu.
Alisema wanawake wengi, hususan wa mijini, wamekuwa
wakitumia vipodozi vyenye kemikali huku wakila vyakula vinavyoandaliwa kisasa
zaidi vikiwa na mafuta mengi au kukaangwa na hivyo kuharibu homoni zao na
kusababisha madhara mbalimbali.
Dk. Mandai alisema matumiz ya vipodozi sit u yana athari
ya kuwafanya wanawake waote ndevu, bali wengi wao wanaopata ujauzito hujifungua
kwa njia ya upasuaji.
“Dawa ya nywele wanayotumia pamoja na vipodozi vyenye
kemikali huchangia kwa kiasi kikubwa kuota ndevu. Katika hili la vipozozi
tambua kuwa chochote kinachokuwa juu ya ngozi ya binadamu kina uwezo wa
kusambaa mwilini na kusababisha madhara mbalimbali,” alisema Dk. Mandai.
Akitolea mfano, alisema zamani wanawake, wakiwemo
wajawazito, walikuwa wanakula vyakula vya asili na kwamba walizuiwa hata kula
mayai, hali iliyokuwa ikiwasaidia wengi wao kujifungu kwa njia ya kawaida.
“Kuna wakati wajawazito 10 wanakuwa wamelazwa hospitali,
kati yao pengine wawili tu ndiyo wanaweza kujifungua kwa njia ya kawaida…
wengine wanafanyiwa upasuaji,” alisema.
Aliongeza kuwa tatizo hilo linaweza kupungua kwa kiasi
kikubwa iwapo wanawake watabadilika na kupenda vitu vya asili na kuacha kuiga
utamaduni wa kimagharibi ambao una athari kubwa kwao.
“Ushauri wangu ni kwamba tuache kupeperusha bendera ya
umagharibi (kuiga tamaduni za kigeni), tudumishe mila zetu ikiwemo kula vyakula
vya asili, matatizo haya yatapungua kwa kiasi kikubwa,” alisema Dk. Mandai.
Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA),
Gaudensia Simwanza alinukuliwa wakati mmoja akisema mamlaka hiyo imepiga
marufuku vipodozi vyote vyenye viambata sumu, lakini watu wanaendelea
kuvitumia.
“Madhara yake ni makubwa, mwanamke mjamzito ni rahisi
kuzaa mtoto tahira au mimba ikatoka,” alisema huku daktari wa magonjwa ya ngozi
wa kituo cha Afya Centre, Isaack Maro akisema wanawake wanaotumia vipodozi
vyenye viambata sumu huathirika kwa kiasi kikubwa bila kujijua.
Alisema madini ya zebaki yanayotumika katika vipodozi
vingi hayatoki kwa urahisi mwili kwani hujazana mwilini kwa muda mrefu na
kusababisha maradhi.
CHANZO: Jambo Leo Septemba 23,2013
0 comments:
Post a Comment