WAASI WA SELEKA WATWAA MIJI MIWILI

Seleka spokesman Eric Massi
Msemaji wa Waasi wa Seleka, Eric Massi




Waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamepambana na vikosi vya serikali katika eneo la kasikazini mwa nchi hiyo na kutwaa miji miwili.


Jana Alhamisi, afisa mmoja wa Serikali alithibitisha kuwa waasi wa muungano wa Seleka umeichukua miji miwili kaskazini mwa nchi hiyo.


Waasi hao walianza kuuteka mji wa Bouca, wenye uwanja wa ndege unaopatikana kiasi cha kilometa 300 (maili 240) kaskazini mwa mji mkuu Bangui,  na kisha wakautwaa mji wa Batangafo, kilometa 100 (maili 62) kaskazini. 

Msemaji wa Seleka, Eric Massi, ambaye kwa sasa yuko nchini Ufaransa, alisema kuwa waasi hao hawatakubali pendekezo la Rais Francois Bozize wa nchi hiyo kuhusu kuwaachia huru wafungwa wa kundi hilo la Seleka. 

Siku ya Jumatano, televisheni ya serikali ilitangaza matangazo mawili ya rais ya kuwaacha huru wafungwa wa kisiasa, kuondosha hali ya hatari na kuondosha vikwazo vya barabarani vinavyolindwa na wapiganaji wanaomtii Bozize.


"Htuna imani tena na ahadi za Bozize. Tunamtaka ajiuzulu, vinginevyo tunamuondosha kwa nguvu," msemaji wa Seleka alisema kwa njia ya simu siku ya Alhamisi.



Massi aliongeza kusema kuwa wapiganaji wa Seleka walikutana na upinzani mdogo kutoka kwa vikosi vya serikali mjini Bouca, na walifanikiwa kuwakamata wanajeshi watatu wa serikali na magari mawili ya kijeshi.


Siku ya Jumatano, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilielezea "wasiwasi mkubwa" kuhusu kuibuka kwa mgogoro nchini humo katika taarifa iliyosomwa na Rais wa Baraza la Usalama, Vitaly Churkin katika mkutano na vyombo vya habari.


Mnamo Januari 11, rais wa nchi hiyo na wawakilishi wa waasi waliasaini makubaliano mjini  Libreville, Gabon baada ya siku tatu za mazungumzo yaliyosimamiwa na nchi jirani.



Chini ya makubaliano hayo, baadhi ya viongozi wa upinzani na wanachama wa muungano wa Seleka walipewa nyadhifa kadhaa muhimu katika serikali.


Waasi wamekuwa wakiituhumu serikali kutotekeleza makubaliano hayo, na wametaka kuachiwa huru kwa wafungwa wao.


Waasi wa Seleka walianza hujuma dhidi ya serikali mwezi Desemba 2012.


Jamhuri ya Afrika ya Kati ina utajiri mkubwa wa maliasili za madini kama vile dhahabu na almasi. Lakini, kama ilivyo kwa nchi nyingi za Kiafrika, nchi hiyo inakabiliwa na umaskini wa kutisha na imekumbwa na mlolongo wa uasi na mapinduzi tangu ilipopata uhuru mwaka 1960.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment