WAARGENTINA WAGAWANYIKA KUHUSU UTEUZI WA PAPA MPYA



Cardinal Jorge Mario Bergoglio(Pope Francis I) washing the feet of 12 recovering drug addicts at a rehabilitation center in Buenos Aires, Argentina on the Holy Thursday In 2008
Kadinali Jorge Mario Bergoglio(Papa Francis I) akiosha miguu ya vijana 12 waliopona dhidi ya matumizi ya madawa ya kulevya katika kituo cha urekebishaji tabia mjini Buenos Aires, Argentina mwaka 2008



UTEUZI wa aliyekuwa kadinali wa Argentina, Kadinali Jorge Mario Bergoglio kuwa kiongozi wa kanisa Katoliki duniani umepokewa kwa mitazamo tofauti miongoni mwa wananchi wa Argentina.

Siku ya Jumatano, Kadinali Bergoglio, mwenye umri wa miaka 76, kutoka Argentina alitangazwa kuwa papa mpya wa Kanisa Katoliki, akichagua jina la upapa la Papa Francis I.
Waargentina wengi wanamsifu Francis I kwa juhudi zake za kupambana na umaskini, msimamo wake wa kihafidhina na mfumo wa maisha yake.

Hata hivyo, raia wengine wa Argentina wanadhani kuwa papa anakabiliwa na historia tata inayohusisha ushiriki wa Kanisa nchini humo na udikteta wa kijeshi wa miaka ya 1976-1983 na kuhoji mchango uliotolewa na Bergoglio kama mkuu wa kundi la Jesuit miaka ya 70.

Kipindi hicho, watu 30,000 walinyongwa, kuuawa na kuteswa na jeshi.

Papa huyo wa kwanza kutoka nje ya Ulaya katika miaka ya karibuni na ambaye pia ni papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini amekuwa na uhusiano mbaya na uongozi wa chama tawala nchini Argentina cha Front for Victory.

Nestor Carlos Kirchner, rais wa zamani na aliyekuwa mume wa rais wa sasa wa nchi hiyo Cristina Fernandez, alimuita Bergoglio kama “mwakilishi halisi wa upinzania.”

Mwaka 2010, mvutano uliibuka kati ya Kanisa Katoliki nchini Argentina na serikali ya nchi hiyo, baada ya bunge kupitisha sheria inayoruhusu ndoa za jinsia moja, mradi ulioibuliwa na kuhubiriwa na serikali ya kitaifa.

Rais Fernandez mwenye sera za mrengo wa kushoto, alimpongeza rasmi Askofu huyo wa zamani wa mji wa Buenos Aires, lakini akamtaka kuhubiri “haki na usawa” na “udugu baina ya dini mbalimbali.”

Alimtaka papa huyo “kupeleka ujumbe wa nchi zinazoinukia kwenda kwa mataifa yenye nguvu ulimwenguni” akiwa kama papa kutoka Amerika ya Kusini.

“Ninatarajia kuwa Bergoglio atawajibika kwa masikini ulimwenguni, kubainisha ufisadi ambao umeibuliwa ndani ya Vatican na kupambana dhidi ya janga hatari la udhalilishaji wa kingono katika Kanisa Katoliki. Ninatarajia ataifanya kazi hiyo na kutoa majibu ya vipaumbele hivi, alisema mbunge wa Argentina Guillermo Carmona.

Viongozi wa Jumuiya ya Waislamu nchini Argentina, ambao wanaunga mkono utawala wa Rais Fernandez, wamekiri kuwepo kwa tofauti baina ya papa huyo mwenye umri wa miaka 76 na serikali, lakini waliukaribisha uteuzi wake kama alivyofanya Rais.

Wakati huo huo, Katibu wa mawasiliano ya Umma na msemaji wa Rais, bwana Alfredo Scoccimarro, amethibitisha kuwa Rais Cristina Fernandez utahudhuria kuapishwa kwa Papa Francis, Machi 19.

Papa Francis anachukua nafasi ya Papa Benedicto XVI kama kiongozi wa kiroho wa waumini wa Kanisa Katoliki duniani.

Mnamo Februari 11, Benedict XVI mwenye umri wa miaka 85 alitangaza uamuzi wake wa kujiuzulu, akisema kuwa hakuwa na uwezo tena wa kutekeleza majukumu yake kutokana na umri wake. Alijiuzulu rasmi Februari 28, na kuwa papa wa kwanza kujiuzulu ndani ya miaka 600.

Ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa na gazeti la Italia la La Repubblica, ilisema kuwa papa huyo aliamua kujiuzulu baada ya wachunguzi wa ndani ya kanisa kumtaarifu kuhusu mlolongo wa uhaini, rushwa na ushoga wa chini kwa chini ndani Vatican.

Papa mpya anakabiliwa na mzigo wa matatizo yaliyokithiri ikiwemo tuhuma za udhalishaji kingono unaoichafua Vatican na tishio la mitazamo inayopinga dini.

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment