MAKUNDI YA WAASI YAPAMBANA

M23 rebels (file photo)
Waasi wa M23



Waasi wa kundi la M23 limewafurusha wapiganaji wanaomtii mbabe wa vita Jenerali  Bosco Ntaganda na kuyadhibiti maeneo yote yaliyokuwa yakishikiliwa na kikundi hicho mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.



Jana Jumamosi, vyanzo vya habari kutoka ndani ya Umoja wa Mataifa na kundi la M23 vilieleza kuwa mamia ya askari wa Ntaganda wamekimbilia nchini Rwanda au kujisalimisha kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa baada ya kushindwa na waasi wa M23.


Mapigano hayo yalizuka mnamo Februari 28 baada ya kiongozi wa kijeshi wa M23 Sultani Makenga kumfukuza kiongozi wa kisiasa wa kundi hilo, Jean-Marie Runiga, kwa tuhuma za kudaiwa kuwa na mafungamano na Ntaganda, jambo lililopelekea wapiganaji hao kushambuliana wao kwa wao. Runiga, pamoja na wapiganaji wengi wanaomtii, waliamua kujiunga na upande wa Ntaganda. 

Ntaganda, anayejulikana kama nom de guerre “mkomeshaji” kutokana na vitendo vyake vya kikatili, amekuwa akitafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya binaadamu tangu mwaka 2006 kwa tuhuma za uhalifu wa kivita kwa kuwasajili na kuwapa mafunzo ya kijeshi  watoto chini ya miaka kumi na tano na kuwatumia katika vita.


Runiga ni miongoni mwa wale waliokimbilia Rwanda: “Nimekuja hapa kwa sababu hali imezidi kuwa mbaya katika uwanja wa mapambano. Nimependa kuyaokoa maisha yangu," alisema. "Kwa sasa, nimekuja kutafuta hifadhi."


Siku kadhaa zilizopita, idadi kubwa ya waasi, wakiwemo maafisa wandamizi, wamejisalimisha kwa walinda amani wa umoja wa mataifa, alisema afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

“Habari ya Bosco na Runiga imefikia mwisho,” alisema. 

“Tumeshinda, tumeshinda vita,” msemaji wa M23 Kanali Vianney Kazarama alisema. 

“Tunasafisha eneo hili na kuwaweka askari wetu kwenye maeneo muhimu," alisema. "Tumemaliza kazi."

Aliendelea kusema kuwa siku ya Jumamosi waasi wa M23 wameuteka mji wa Kibumba, kilometa 30 kaskazini mwa Goma. 

Msemaji huyo wa M23 alieleza pia kuwa Ntaganda na wapiganaji wake wapatao 200 walikimbilia msituni huku mamia wengine wakikimbilia nchi jirani ya Rwanda na kwa uchache saba waliuawa.


Wakati huo huo, msemaji wa Serikali ya Kongo, Lambert Mende alisema, “Tunafuatilia hali hiyo kwa ukaribu sana. Kitu pekee tunachotaka ni kuona Ntaganda anakamatwa."


Makundi kadhaa yenye silaha, ikiwemo M23, wanaendesha harakati zao za uasi mashariki mwa Kongo na wanapigania kuidhibiti nchi hiyo kubwa yenye maliasili za madini, kama vile dhahabu, urani, coltan, ambayo hutumika katika utengenezaji wa vifaa vingi vya elektroniki, ikiwemo simu za mkononi.

Waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma Novemba 20, 2012 baada ya walinda amani kuondoka  katika mji huo wenye wakazi milioni moja. Wapiganaji wa M23 waliondoka katika mji huo Desemba 1,2013 baada ya makubaliano ya kusimamisha mapigano.


Waasi wa M23 walijiondoa katika jeshi la Kongo mwezi Aprili 2012 kupinga kile walichodai kuwa ni mwenendo mbaya ndani ya jeshi la Taifa (FARDC). Walikuwa wamejumuishwa katika jeshi chini ya mkataba wa amani uliosainiwa mwaka 2009.


Tangu mwezi Mei 2012, takriban watu milioni 3 wameyekimbia makazi yao katika eneo la mashariki mwa Kongo. Takriban watu milioni 2.5 ni wakimbizi wa ndani, huku zaidi ya watu 460,000 wamekimbilia katika nchi za Rwanda na Uganda.


Kongo imekuwa ikikabiliwa na matatizo matatizo kwa miongo kadhaa, kama vile umaskini uliokithiri, miondombinu mibovu, na vita katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambavyo viliibuka tangu mwaka 1998 na kugharimu maisha ya zaidi ya watu milioni 5.5.

Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment