KIBANDA ALITESWA NA MAJASUSI

Rais Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wakimjulia hali Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, akiwa hospitalini Afrika Kusini





SASA kuna dalili zinazoonyesha kuwa utekelezaji wa mpango wa kumteka na kumtesa kinyama Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, ulifanywa na watu waliopata mafunzo wanayopewa maofisa Usalama wa Taifa, Makachero wa Jeshi au wale wa Polisi, Mtanzania Jumapili linaripoti.

Duru za uchunguzi za Mtanzania Jumapili zimebaini kuwa ni watu wenye mafunzo maalumu ya kutesa na kuua, waliyopata katika vyuo vya kijasusi wenye uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi utesaji wa aina aliyofanyiwa Kibanda au ule wa awali uliotekelezwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.

Makachero kadhaa waliobobea, waliozungumza na gezeti hili kuhusu aina ya mateso ambayo yamepata kutolewa kwa baadhi ya Watanzania (akiwemo Kibanda) na kundi la watu ambalo hadi sasa halijafahamika, walieleza kuwa kwa ufahamu wa kazi yao ya ukachero, watu waliomteka na kumtesa Kibanda ni ama maofisa usalama, Makachero wa Jeshi au Polisi au watu waliopata mafunzo yanayolingana na watu wa kada hizo.

Walisema wanaamini hivyo kwa sababu staili iliyotumika kumteka na kisha kumtesa, muda uliotumika kutekeleza utekaji na utesaji ni ule unaofundishwa katika vyuo vya kijasusi vilivyoko katika nchi za Magharibi na Asia ambavyo ni maalumu kwa ajili ya maofisa wa kijeshi na wale wa usalama.

Kachero mwingine mstaafu aliyeulizwa kuhusu aina hiyo ya kuteka na kutesa alisema ni jambo lililo wazi kuwa watu ambao wamekuwa wakitekeleza unyama huo wana mafunzo ya kazi hiyo ambayo hutolewa kwa watu maalumu hususan maofisa usalama na wanajeshi.

Alisema staili iliyotumika kumteka na kumtesa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Steven Ulimboka, ndiyo iliyotumika kwa asilimia 95 kwa Kibanda, ambayo kwa mwana usalama yeyote, akisimuliwa au kumuona mtu aliyeteswa kwa namna hiyo, anajua kazi hiyo imefanywa na watu wa aina gani.

“Jambazi wa kawaida au mtu mwingine tu aliyeamua kufanya unyama siyo rahisi kwake kung’oa meno, kunyofoa kucha, kukata vidole, kuvunja mishipa na kutoboa macho bila kuwa na utaalamu wa kufanya kazi hiyo kwa wepesi na ufanisi kama inavyotokea sasa.

“Anaweza akafanya hivyo lakini si kwa ufanisi kama ilivyo kwenye matukio ya Kibanda na Ulimboka. Unajua, kuna mambo ambayo yako wazi, kazi za kitaalamu zinajulikana kuwa zimefanywa kitaalamu na za kienyeji nazo zinajulikana. Haya mambo yanafanywa na watu wenye ujuzi wa kazi hiyo, sasa hatujui ni akina nani, lakini ukweli unabaki hivyo kuwa watu hawa wana utaalamu wa kutesa na kuua,” alisema.

Utafiti iliofanywa na Mtanzania Jumapili umeonyesha kuwa makachero wa mashirika makubwa ya kijasusi duniani na hasa wa Nchi za Magharibi na zile za kikomunisti, hutesa watu waliowakusudia kwa sababu mbalimbali kwa staili kama aliyoteswa nayo Kibanda na Ulimboka.

Mateso ya aina hii hutolewa kwa watu wanaolazimishwa kutoa taarifa za siri au kukiri jambo walilolificha moyoni.

Kwa mujibu wa mtandao wa plisonplanet.com, utesaji wa kukata viungo vya binadamu hutekelezwa ili kumlazimisha mtu atoe taarifa au akiri jambo analolificha na kwamba hata baadhi ya mataifa ya Asia na Afrika hutumia mbinu hizi yalizozipata kutoka Nchi za Asia na Magharibi.

Taarifa za utesaji wa aina hiyo zilizo katika mitandao mbalimbali inayofuatilia mienendo ya kiintelijensia zinaeleza kuwa staili hiyo ya kinyama kutekelezwa kwa binadamu (slow slicing) na ilianzia nchi ya China katika miaka ya 600 AD hadi mwaka 1905 ilipokatazwa. Hata hivyo, inabainishwa kuwa mateso ya aina hiyo bado yapo katika baadhi ya nchi, zikiwemo za Afrika zinazotajwa kuongozwa kidikteta.

Sehemu ya taarifa iliyo katika tovuti hiyo inasomeka kuwa; ‘katika mateso ya aina hii, mtesaji hutumia kisu chenye ncha kali kutoa jicho, kung'oa au kukata masikio, pua, ulimi, vidole, na kabla ya kuendelea na hivyo hukata vipande vidogo vya nyama kutoka sehemu za mapaja na mabega. 

‘Mchakato mzima wa mateso ya namna hii huendelea kwa karibu siku tatu ili kumlazimisha mteswaji kueleza au kukiri jambo na inakadiliwa kuwa mteswaji hukatwa karibu mikato 3,600 kabla ya kufariki dunia.’

Katika uchunguzi huo, pia tumebaini kuwa aina ya mateso ya kung’oa watu kucha pia yamekuwa yakitumiwa na watu wa Usalama wa Taifa nchini Iran, ambako wao hutumia mashine kumnyofoa kucha. 

Wakati uchunguzi wa Mtanzania Jumapili ukibaini hayo, kumekuwa na hali ya hofu kwa jamii kuhusiana na matukio ya utekaji na utesaji kinyama yanayotekelezwa sasa kwa baadhi ya watu maarufu hapa nchini wanaotambulika kuwa na misimamo inayokinzana na ile ya serikali.

Tukio la kwanza lililoibua hofu ya kuwepo kwa kikundi maalumu chenye mafunzo ya kutesa na kuua ni lile la Dk. Ulimboka, ambaye akiwa katikati ya mzozo mkali na serikali kwa wadhfa aliokuwa nao wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, alitekwa, akateswa vibaya na kwenda kutupwa katika msitu wa Pande, akiwa nusu maiti.

Dk. Ulimboka aliteswa kwa kupigwa mateke, ngumi, kung’olewa meno, kunyofolewa kucha na kuvunjwa baadhi mifupa ya mwili wake, zikiwemo mbavu. Mateso kama hayo ndiyo aliyoteswa nayo Kibanda. 

RAIS KIKWETE AMJULIA HALI KIBANDA

Katika hatua nyingine, juzi Rais Jakaya Kikwete alimtembelea Kibanda katika hospitali aliyolazwa ya Mill Park, iliyopo mji wa Johannesburg, nchini Afrika Kusini kwa lengo la kumjulia hali.

Rais Kikwete alikuwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana.

Habari zinaeleza kuwa Rais Kikwete alitumia fursa ya kuhudhuria Mkutano wa Viongozi wa Vyama vilivyokuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubaguzi wa rangi, unaofanyika nchini humo, kwenda kumuona Kibanda. 

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa; Kikwete ambaye alizungumza na Kibanda kwa takribani dakika tano, alisema aliongea na Mwajiri wa Kibanda, ambaye alimueleza kuwa suala la matibabu alikuwa akilishughulikia, hivyo kwa upande wao serikali, itaendelea na uchunguzi na kuhakikisha wale wote waliohusika katika tukio hilo wanakamatwa.

KIBANDA AFANYIWA OPERESHENI 

Madaktari bingwa watatu, wakiwemo wa kichwa na jicho, jana walimfanyia operesheni Kibanda, iliyochukua takribani masaa matano na nusu.

Katika operesheni hiyo ya kurekebisha taya na mishipa inayozunguka jicho, hata hivyo madaktari hao walishindwa kuokoa jicho lake na hivyo kuliondoa kwa ajili ya kumuwekea jingine la bandia.

Ripoti ya madaktari kuhusu kile kilichofanyika ndani ya chumba cha operesheni itatolewa leo.

Kibanda alivamiwa na watu wasiojulikana wakati anajiandaa kufunguliwa lango la kuingia nyumbani kwake, Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam Machi 5 mwaka huu na kumjeruhi sehemu kadhaa za mwili wake na kisha kumng’oa meno, kucha na kumjeruhi vibaya jicho lake la kushoto.


CHANZO: MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment