Askofu Mokiwa avamiwa, mlinzi wake taabani


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, amevamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake, Mbezi Luis, eneo la Mashirikiano, jijini Dar es Salaam, ambapo baada ya kumkosa walimjeruhi mlinzi wake.

Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili, na kuthibitishwa na Askofu Mokiwa mwenyewe, zinaeleza kuwa watu hao watatu ambao mpaka sasa hawajafahamika, walifika nyumbani kwake hapo juzi majira ya saa tisa usiku wakitaka kumuona askofu huyo.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, mmoja wa watu wa karibu na askofu Mokiwa alisema watu hao walifika kwa lengo la kutaka kuingia ndani ili waweze kumuona, hali iliyomfanya mlinzi kuwazuia.

“Wale watu walipofika kwa mlinzi walimuuliza kuwa askofu yupo.. mlinzi akawajibu kuwa hayupo, wakamuuliza tena mama je (mke wa askofu), akawajibu kuwa wote hawapo, baada ya kujibiwa hivyo walianza kumpiga mlinzi kwa madai kuwa hataki kuonyesha ushirikiano, walimpiga na kumjeruhi vibaya kwa mapanga na hadi sasa amelazwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha,”,kilisema chanzo hicho.

Alisema mlinzi huyo aliyetambulika kwa jina la Fred, anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 45, alipigwa hadi kuzimia kabla ya watu hao kutokomea kusikojulikana.

Habari zilizothibitishwa na mtu mmoja wa karibu na Askofu huyo zinaeleza kuwa, mlinzi huyo aligoma kuwaambia ukweli watu hao kwa sababu alikwishaonywa kuwa makini na wageni wa aina yoyote wanaofika nyumbani hapo kumuulizia Mokiwa.

Mtoa habari wetu huyo aliliambia gazeti hili kuwa wakati mlinzi huyo akivamiwa na kucharangwa mapanga, Askofu Mokiwa pamoja na mke wake walikuwemo ndani ya nyumba lakini hawakuweza kusikia lolote, kutokana na lango la kuingia nyumbani kwake kuwa mbali na nyumba.

“Askofu alishamtahadharisha mlinzi kwa sababu wiki mbili zilizopita alishatoa taarifa polisi kuhusiana na vitisho alivyokuwa akipewa na watu wasiojulikana, kikubwa kilichosaidia ni kwamba nyumba ya askofu iko umbali kidogo, lakini wangemdhuru,” alisema mtoa taarifa wetu huyo.

Katibu Mkuu wa kanisa hilo, Dk. Dickson Chilongani, alisema wamepokea taarifa hizo kwa masikikito na kwamba wanasubiri taarifa rasmi kutoka kwa askofu ili wazifanyie kazi.

“Tayari tumepata taarifa, lakini nimejaribu kumtafuta askofu Mokiwa nimeambiwa kwamba anahojiwa na vyombo vya usalama, tunasubiri amalize tuzungumze naye ili tulifuatilie kwa ukaribu suala hili, kwani ni tukio la kushtusha,” alisema Chilongani.

MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Askofu Mokiwa kwa njia ya simu ambapo alithibitisha juu ya habari za kuvamiwa nyumbani kwake na akamtaka mwandishi wa gazeti hili amtafute baada ya dakika 40.

Mwandishi wa gazeti hili alimtafuta tena Mokiwa baada ya dakika 40 kupita simu yake, iliita bila mafanikio na alipotumiwa ujumbe mfupi wa kumkumbusha aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kuwa ana ugeni wa serikali na kulitaka gazeti hili limpigie baada ya dakika 45.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyella, alisema amesikia taarifa hizo, lakini hajazipokea rasmi ofisini kwake.

“Ni kweli hata mimi nimesikia, lakini hazifafika ofisini kwangu rasmi, nitafute baadaye naweza kuwa na taarifa sahihi, kwa sababu wao wako Mbezi, inawezekana hizo taarifa zipo huko Mbezi katika kituo cha polisi cha Mbezi kwa Yusuph,” alisema Kamanda Kenyella.

Baadaye Kamanda Kenyella alipotafutwa kuthibitisha tukio hilo, simu yake iliita bila kupokelewa, ambapo MTANZANIA Jumapili ilipata taarifa kwamba wapelelezi wakiongozwa na Kamanda Kenyella, walikwenda nyumbani kwa Askofu Mokiwa kwa ajili ya kufuatilia tukio hilo.

CHANZO: MTANZANIA
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment