HAYA NDIYO MADAI YA ODINGA MAHAKAMANI


NA 
DOROTHY JEBET, NAIROBI


Raila Amollo Odinga amekuwa akipigania haki za wanyonge Kenya kwa muda mrefu. Amepigania demokrasia na ametaabika kwa kujiweka mbele katika harakati za kukomboa Kenya kwa mara ya pili. Miaka ya 80 alifungwa miaka tisa na utawala wa kiimla wa Rais Daniel arap Moi.
Wakenya wengi kwa hivyo wamekuwa wakitarajia kwamba siku moja angewaongoza na kuwapeleka katika nchi ya Kanaani wafurahie maziwa na asali.  Hayo hayajatokea kwa sababu ya anachoeleza kuwa kura kuibwa au kuwa na dosari chungu nzima.
Mara ya kwanza ilikuwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 ambapo ingawa Odinga alidai ameshinda, ushindi wake uliibwa na Rais Mwai Kibaki akaapishwa usiku. Ghasia na mapigano yalifuata na wengi waliuawa.
Wakati huo, Odinga alishauriwa na vibaraka wa Kibaki aende kortini ikiwa ana ushahidi kwamba kura ziliibwa. Odinga hakufanya hivyo kwa kuwa hakuwa anaamini ka mahakama za Kenya. Baadaye, alikubali kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya Kibaki.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umepita na Odinga hakushinda, lakini tofauti na awali, mara hii ana imani na mahakama, ameamua kuwasilisha maombi ya kutaka Mahakama ya Juu zaidi ibatilishe uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wa kumtangaza Uhuru Kenyatta kama mshindi urais.
Odinga, aliyekuwa akigombea urais kwa tiketi ya Muungano wa Coalition For Reform and Democracy (CORD) anadai kwamba Uhuru alitangazwa mshindi baada ya kuongezewa kura na IEBC, jambo alilosema ni kinyume na sheria.
Ombi lake kwa mahakama inasema kwamba uchaguzi mkuu uliofanywa Machi 4 haukuwa wa haki na huru na kwa hivyo hakuna Serikali inayoweza kuuundwa kwa msingi wa uchaguzi mkuu uliosheheni udanganyifu.
Anasema Uhuru Kenyatta na William Ruto kamwe hawawezi kuwa wamechaguliwa na Wakenya wengi kama iliyotangazwa na IEBC wiki moja unusu iliyopita.

Pia anadai kuwa orodha ya wapiga kura waliosajiliwa ilibadilishwa zaidi ya mara moja kwa lengo la kutatiza ili isijulikane ni orodha ipi ilitumiwa katika upigaji kura.

Kwenye gazeti rasmi la Serikali baada ya zoezi la usajili Desemba 18, 2012 kulikuwa na wapiga kura 14,267,572 lakini wakati wa kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu IEBC ilisema wapigaji kura waliosajiliwa ni 14, 352,533.
Anahoji kwa nini IEBC iliongeza idadi ya wapiga kura kwa kuwasajili watu wengine 85,000 jambo linalokinzana na kanuni za uchaguzi na sheria za IEBC. 

Ya tatu ni kwamba, mashine za kupigia kura maarufu kama Boimetric Voter Registration (BVR) na mashine zingine maalumu za kielektroniki zilizokuwa zimepangwa zitumike kuhesabu na kutuma matokeo ya kura kutoka maeneo yote ya nchi yalikosa kufanya kazi siku ya kupiga kura.

Ilikuwa vigumu kwa IEBC kuwaelezea Wakenya sababu za mashine zilizokuwa zimejaribiwa na zikafanya kazi kuharibika ghafla. Isitoshe, pesa za umma zipatazo bilioni 9 zilitumiwa kuzinunua.
Baada ya mashine kuharibika, ililazimu IEBC kuhesabu kura kwa mkono jambo lililosababisha hesabu mbaya na kubadilishwa kwa matokeo mengine kumfaidisha Uhuru na Ruto.

Sababu ya nne ambayo Cord imeenda kortini ni kwamba, wanataka kujua kwa nini Fomu namba 36 iliyotangazwa na IEBC ilikuwa na dosari nyingi za matokeo.
Tofauti hizo katika fomu 36 hazingeweza kufanyika ila tu kwa njia ya kujaribu kudanganya na hali ya watu fulani kuongeza karatasi bandia za kupiga kura, watu kupiga kura zaidi ya mara moja, kubadilisha mipaka ya kupiga kura kuongeza wapigaji kura wakati wa kuhesabu kura katika matokeo ya kitaifa.
Ombi jingine la Odinga linasema kwamba kulikuwa na dosari katika zoezi la kupiga kura katika maeneo kadhaa kama vile Mlima Elgon na Bomet Mashariki, Langata na Aldai miongoni mwa mengine.
Linasema matokeo ya urais katika Fomu 36 yaliyotangazwa na IEBC yalikuwa tofauti kabisa na yale yaliyohesabiwa na kukubaliwa awali haswa kuhusiana na matokeo yaliyotumwa kutoka eneo la Webuye Mashariki na Magharibi, Igembe na maeneo mengine mengi.
Cord pia inataka kujua kwa nini wapiga kura waliosajiliwa katika vituo vya kupigia kura waliongezeka katika Fomu 34 kinyume na idadi ya wapiga kura walioorodheshwa katika Fomu 36. Dosari hiyo iligunduliwa katika maeneo 10 nchini.
Isitoshe anasema, Fomu 36 zaidi ya mbili zilionyesha matokeo tofauti katika maeneo Bunge ya Kikuyu, Juja, Chuka na Thika.
Linasema mabadiliko yalifanyiwa Fomu 36 bila sababu katika maeneo bunge ya Kiambaa na Limuru. Yote haya ni maeneo ambayo Uhuru ana wafuasi wengi.
Pia kura zaidi ambazo hazikuharibika zilizopigwa katika maeneo mengine ya uwakilishi bungeni yalionyeshwa katika Fomu 36 kuliko Fomu 34.
Odinga anateta kwamba Fomu mbili za 36 za eneo moja ziliwasilishwa katika makao makuu ya kuhesabu kura za kitaifa. Alitoa mfano wa eneo la Mathira ambalo ilikuwa na Fomu 36 mbili ilhali ni kituo kimoja.
Mbali na hayo, kuna maswali mengi yasiyo na majibu kuhusiana na kwa nini IEBC na chama cha The National Alliance (TNA) cha Uhuru zikatumia huduma za kampuni ya utoaji huduma za kimtandao ya Kencall. Je, hii ilkuwa bahati mbaya au mpango wa kuhujumu matokeo ya kura?
Odinga anasema kwa kutumia huduma za Kencall pamoja inaonyesha kwamba Uhuru alikuwa an uwezo wa kufikia habari zozote za muhimu za IEBC kuhusiana na zoezi hili muhimu la upigaji kura.
Anaamini kwamba IEBC na mweyekiti wake, Isaack Hassan walikosa kuunda mifumo isiyo na dosari au tashwishi na iliyo salama, wazi na huru.
Zaidi ya hayo anasema kwamba, wawakilishi wote wa Cord walikosa kuhusishwa kwa njia moja au nyingine katika masuala yote ya utangazaji wa matokeo na hesabu zake.
Anasema kinyume na matangazo ya IEBC, Uhuru hakupata zaidi ya nusu za kura zote zilizopigwa na kwa hivyo anataka cheti cha ushindi wa urais kilichopewa Uhuru Machi 7 kifutiliwe mbali na korti.

Ikiwa mahakama itakubali hoja hizo, inaweza kutengua matokeo na uchaguzi mkuu mwingine kufanyika ndani ya siku 60 baada ya uamuzi wa mahakama. Hii ni kulingana na vipengee vya Katiba ya nchi.
Ikiwa mahakama itaamua kwamba kuwe na uchaguzi mwingine, wagombea wote wanane wa urais watatarajiwa kuwa mbioni kutafuta kura tena na mtu mwingine yeyote anayetaka kugombea urais. Uchaguzi kama huu utakuwa tofauti na ule ambao Odinga na Uhuru pekee wanashindana katika awamu ya pili.
 CHANZO: MWANANCHI
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment