Tanzania imesisitiza uamuzi wake wa kuendelea na mpango
wa kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji
(Stiegler's Gorge Hydro Power Project) yaliyopo ndani ya Pori la Akiba la
Selous mbele ya wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia kutokana na umuhimu wake
kwa maendeleo ya Watanzania.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mkutano wa 41 wa
wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendeshwa na Shirika la Elimu, Sayansi
na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambao unaendelea katika Jiji la
Krakov nchini Poland, Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya
Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliwaeleza wajumbe wa
mkutano huo kuwa mpango huo ulikuwepo katika ajenda ya Serikali ya Tanzania
tangu miaka ya 1960's na kwamba ukubwa wa eneo litakalotumika kutekeleza mradi
huo ni asilimia tatu tu ya eneo lote la pori hilo ambalo lina ukubwa wa
kilometa za mraba 50,000.
Aliongeza kuwa, “Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 1982
wakati pori hili (Selous) limewekwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia,
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Asili (IUCN) liliutambua mradi huo
wa Stiegler's Gorge kutokuwa na madhara makubwa katika uharibifu wa mazingira
ukizingatia ukubwa wa pori hilo na eneo litakalotumika kujenga mradi huo”.
Aliwaeleza wajumbe hao kuwa, Serikali ya Tanzania
inatekeleza sera ya kujenga uchumi wa viwanda hali inayopelekea kuwa na
mahitaji makubwa ya nishati ya umeme hivyo kwa kuzingatia vyanzo vilivyopo
imekuwa ni muhimu sasa kufikiria tena ujenzi wa mradi huo kama chanzo kingine
muhimu cha nishati kuwezesha kufikia azma hiyo.
Alisema mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme nchini
kufikia asilimia 144.8 hivyo kuondoa upungufu wa nishati uliopo kwa sasa na
pindi utakapokamilika utawanufaisha watanzania wengi wanaoishi bila umeme ikiwa
ni pamoja na kukidhi mahitaji yake ya kuendesha viwanda.
Meja Jenerali Milanzi alilazimika kutoa maelezo hayo kwa
kamati hiyo ili kuweka bayana dhamira ya dhati Serikali ya Tanzania ya
kuendelea na ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya maendeleo endelevu huku akitoa
rai kwao kuwa Serikali bado ipo tayari kwa mazungumzo ya namna bora ya
kutekeleza mradi huo kwa faida ya jamii, uchumi na mustakbali bora wa mazingira
ya hifadhi ya Selous na taifa kwa ujumla.
“Kwa kutumia teknolojia bora zilizopo, mipango imara na
usimamizi thabiti, mradi huu utakua na faida kubwa kwa taifa ikiwa na pamoja na
kuboresha maisha ya watu maskini na jamii kwa ujumla bila kuathiri mazingira
yanayotoa faida hizo”, alisema Milanzi.
Hapo awali, kabla ya mkutano huo, ujumbe wa Tanzania
ukiongozwa na Katibu Mkuu huyo ulifanya mazungumzo na Maafisa Waandamizi wa
Kituo cha Urithi wa Dunia na Bodi za Ushauri ya kituo hicho na kuwasilisha kwa
maandishi msimamo wa Tanzania kuhusu ujenzi wa mradi huo.
Tanzania ilipinga vikali rasimu ya azimio No. 41 COM 7
A.17 aya ya 7 ambalo liliitaka kusitisha kabisa (to permanently abandon) ujenzi
wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler's Gorge
Hydro Power Project). Baada ya tamko la Tanzania kupinga azimio hilo kipengele
hicho kilifanyiwa marekebisho ipasavyo na neno “to permanently abandon”
(kusitisha kabisa) liliondolewa katika azimio hilo kupisha majadiliano zaidi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi wanachama zilizosaini
mkataba wa urithi wa Dunia wa mwaka 1972 huku ikiwa na maeneo saba
yaliyorodheshwa katika urithi huo ikiwepo Pori la Akiba la Selous, Hifadhi ya
Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mji Mkongwe (Zanzibar),
Hifadhi ya Ngorongoro na Michoro ya kondoa na Kilwa Kisiwani. Aidha, ni
mwanachama wa Kamati ya Urithi wa Dunia kwa kipindi cha miaka minne hadi mwaka
2019.
Tokea ijiunge na kamati hiyo mwaka 2015, Tanzania imekua
na msimamo wa kuwa na maendeleo endelevu katika ajenda za mikutano yake pamoja
na miongozo yake ili kuruhusu kuendeleza maeneo ya urithi wa dunia kuweza
kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi bila kuwepo kwa athari kubwa katika
mazingira.
Mkutano huo wa 41 wa wajumbe wa Kamati ya Urithi wa
Dunia unaoendelea katika jiji la Krakov nchini Poland umehudhuriwa na nchi
wanachama 193 na unajadili mambo mbalimbali muhimu kuhusu uhifadhi na ulinzi
maeneo ya urithi wa dunia pamoja na kutangaza maeneo mengine mapya ya urithi wa
dunia yaliyowasilishwa na nchi nyingine wanachama katika mkutano huo.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo ulijumuisha pia
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa ambaye pia ni mjumbe wa kudumu wa UNESCO,
Samwel W. Shulukindo na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na
Utalii. Mkutano huo ulianza tarehe 2
Julai na unategemewa kumalizika tarehe 12 Julai, 2017.
0 comments:
Post a Comment