| Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma |
JOHANNESBURG
Rais Jacob Zuma amewataka raia wa Afrika Kusini
kutoitembelea Israel isipokuwa kwa safari zinazohusiana na “kustawisha amani” katika eneo la
Mashariki ya Kati.
Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wakati wa maadhimisho ya
kumbukumbu ya kuasisiwa kwa chama chake cha African National Congress (ANC) mjini
Johannesburg leo Jumapili, Zuma alisema: "Watu wa Palestina wanaendelea
kupata mateso katika harakati za kudai haki yao ya kujitawala”.
Zuma ambaye pia ni kiongozi mkuu wa ANC, alisema kuwa
chama chake kiliahidi kuendeleza “mshikamano
na kuunga mkono mapambano ya wananchi wa Palestina.”
alisema: "Hatuwashauri kutembelea Israel kwa safari
zisizohusiana na ustawishaji wa amani."
Aidha, Kiongozi huyo wa Afrika Kusini alitoa wito wa
kuwepo mshikamano kati ya makundi ya Kipalestina na kusema kuwa chama chake
kiliunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoilaani
Israel kwa sera zake za makazi ya walowezi.
Wanafunzi, wafanyabiashara na maafisa ambao walikuwa
wakiitembelea Israel wamekuwa wakikosolewa kwa kitendo chao hicho.
Wananchi wengi wa Afrika Kusini, wakiwemo wanachama wa
chama tawala cha ANC wamekuwa wakiiunga mkono waziwazi harakati ya Wapalestina dhidi
ya ukaliaji kimabavu wa utawala wa Israel kwenye maeneo ya Wapalestina.
Waafrika Kusini wengi wanaamini kuwa kinachotokea
Palestina ni sawa na kile kilichowatokea wakati wa zama za ubaguzi wa rangu uliodumu
kwa miongo mingi ambao ulifikia kikomo mwaka 1994.
Aidha, Rais huyo aliitolea wito Marekani kukirejesha
kisiwa cha Guantanamo Bay mikononi mwa Cuba na kuondosha vikwazo vya kiuchumi
dhidi ya nchi hiyo, akisema kuwa ANC "itaendelea kusimama pamoja na
wananchi wa Cuba".
Kiongozi wa zamani wa Cuba, hayati Fidel Castro, aliwahi
kuunga mkono mapambano ya Waafrika Kusini dhidi ya utawala wa wazungu wachache
ambao waliwanyanyasa raia weusi kwa miongo kadhaa.
Zuma alisema pia kuwa ANC itaendelea kushikamana na sera
ya Umoja wa Afrika na kufanikisha azma ya Afrika yenye maendeleo na ustawi.
Rais huyo pia aliitaka jumuiya ya kimataifa kuwasaidia
watu wa Syria kupata suluhisho la amani na la kudumu la mgogoro unaoikabili
nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment