Kiongozi wa Boko Haram aliyeenguliwa, Abubakar Shekau. |
Kundi la Boko Haram la nchini Nigeria limempata kiongozi
mpya. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vyenye uhusiano na kundi hilo, Abu Musab
al-Barnawi, ambaye alikuwa msemaji wa kundi hilo, amechukua nafasi ya Abubakar
Shekau, ambaye ameliongoza kundi hilo tangu mwaka 2009.
Hata hivyo, sababu za mabadiliko hayo hazijawekwa wazi.
Mapema leo Alhamisi, Shekau alitoa ujumbe wa sauti
akisema, “watu wanatakiw akujua kwamba bado tupo,” akionekana kumpinga uamuzi
wa kumuondosha kwenye nafasi ya uongozi wake.
Barnawi amedai kuwa kundi lake limeendelea kuwa imara na
kwamba mapambano yataendelea dhidi ya nchi za Afrika Magharibi.
“Wanafanya juhudi za kutaka kuifanya jamii kuwa ya
Kikristo… wanatumia vibaya hali ya wale walioyakimbia makazi yao kwa sababu ya
vita, wanawapa chakula na makazi na kuwabadilisha watoto wao kuwa Wakristo,”
alisema akikusudia mataifa ya Afrika Magharibi.
Al-Barnawi alisema kuwa kundi hilo litajibu kitisho
hicho kwa kulishambulia kila kanisa watakalolifikia na kuwaua wale (Wakristo)
watakaowakuta humo.
Picha ya Maktaba ikiwaonesha wanamgambo wa kundi la Boko Haram |
Kundi la Boko Haram lilianza uasi nchini Nigeria mwaka 2009
kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo. Mpaka sasa watu wapatao 20,000
wameshapoteza maisha na wengine zaidi ya milioni 2.5 kuyakimbia makazi yao.
Hivi karibuni kundi hilo liliungana na kundi la Dola ya
Kiislamu (Daesh) ambalo linafanya harakati zake za uasi katika nchi za Iraq na
Syria.
Tukio la mwaka 2014 la kutekwa wasichana 276 lililofanywa
na Boko Haram liliifanya dunia kushtuka na kuanza kuwa na itibari juu ya uasi
wa kundi hilo.
Boko Haram imeeneza mashambuli yake kutoka kaskazini
mashariki mwa Nigeria mpaka katika mataifa jirani ya Chad, Niger na Cameroon.
0 comments:
Post a Comment