Jamii ya Waturuki waishio nchini Tanzania jana walitoa
tamko la pamoja kulaani jaribio la mapinduzi lililofanywa na kikundi cha
wanajeshi wanaodaiwa kuwa wafuasi wa mhubiri wa Kiislamu, Fathullah Gulen,
huku wakitoa wito wa kufungwa kwa shule zenye uhusiano na mwanazuoni huyo.
Waturuki hao walikusanyika mbele ya ubalozi wa nchini
hiyo jijini Dar es Salaam kutoa tamko hilo.
“Sisi kama raia na taasisi za Kituruki hapa Tanzania
tunalaani vikali jaribio la shambulizi la kijeshi lililofanywa Julai 15 kwa
lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Uturuki kwa njia za haramu. Tumefurahi
kufahamishwa kuwa jaribio hili limeshindwa na serikali iliyochaguliwa kihalali
imeendelea kuhudumu kwa nguvu zote,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Wakifafanua sababu ya kukusanyika mbele ya ubalozi, watu
hao walisema kuwa wanataka kutangaza utii wao na uungaji mkono kwa Rais Recep
Tayyip Erdoğan na serikali yake.
“Jaribio la mapinduzi ya kijeshi lilifanywa na kikundi
kiitwacho FETÖ ambacho kimekuwa kikifanya harakati dhidi ya serikali ya Uturuki
kwa muda mrefu. Kwa bahati mbaya, kundi hili pia lina shughuli zake nchini
Tanzania kwa jina la Taasisi ya Elimu na Tiba ya Ishik, Shule za Feza na ABITAT
(Muungano wa Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda wa Tanzania na Uturuki). Sisi
kama jamii na taasisi za Kituruki hatufurahishwi na makundi haya na kwamba
wanafanya kazi kwa uhuru katika ardhi ya ndugu zetu, Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,” walisema.
“Tunataraji kuwa serikali ya Tanzania itachukua hatua za
lazima kukomesha shughuli za kundi hili nchini Tanzania,” walisema, huku
wakitoa wito wa wazi kwa serikali kkuzifungia shule zenye uhusiano na kundi
hilo.
Kundi la Harakati ya Gulen linaloongozwa na mhubiri
Fathullah Gulen anayeishi uhamishoni nchini Marekani katika jimbo la Pennsylvania,
linatuhumiwa kupanga njama dhidi ya serikali ya Uturuki, kurekodi kwa siri
mazungumzo ya maelfu ya watu, wakiwemo maafisa wa serikali. Serikali ya Uturuki
imetangaza kuwa kundi hilo ni kitisho kwa usalama wa taifa, na kulitangaza
rasmi kuwa ni kundi la kigaidi.
Maafisa wa serikali wamekuwa wakieleza mara kwa mara
azma yao ya kuendelea kupambana na Harakati ya Gulen kwa njia za kisheria. Wafuasi
wa kundi hilo walipenya katika taasisi za dola kwa lengo la kudhibiti mifumo ya
dola, kurikodi maafisa na kughushi nyaraka za serikali.
CHANZO: Daily Sabah
Kuapata habari kupitia WhatsApp: +255 712 566 595
Kuapata habari kupitia WhatsApp: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment