Nyota wa muziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,
Koffi Olomide, amehukumiwa kifungo cha miezi 18 jela na mahakama moja mjini
Kinshasa bila kutakiwa kulipa faini
yoyote kwa kosa la kumshambulia mmoja wa watumbuizaji wake wa kike mjini
Nairopbi.
Hukumu hiyo imeongeza pigo anguko la kazi yake ambalo
lilianza kwa kumpiga teke mmoja wa wachezaji wake kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa
wa Jomo Kenyatta (JKIA), mjini Nairobi Ijumaa iliyopita. Olomide aliondolewa
nchini humo sambamba na wachezaji wake watatu wa kike.
Mwanamuziki huyo alikamatwa na kuhojiwa mjini Kinshasa, jambo
lililoongeza masaibu kwenye umaarufu wake baada ya kufukuzwa nchini Kenya.
Shirika la habari la Uingereza, BBC, liliripoti kuwa
Olomide alikamatwa kwa amri ya Mwanasheria Mkuu.
Masaibu ya Olomide yamevuka mipaka baada ya Chama cha
Wakulima na Wafanyabiashara wa Zambia kusalimu amri mbele ya shinikizo la umma
na kufutilia mbali maonesho yake ya muziki yaliyokuwa yamepangwa kufanyika
mjini Lusaka.
Chama hicho kilisema kuwa tukio hilo la “kusikitisha”
ndio sababu ya kufutilia mbali ziara ya mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka
60 anayepigania kufikia rekodi ya mkongwe wa muziki wa Kongo Franco (Luambo
Luanzo Makiadi), aliyefariki mwaka 1989, lakini amekuwa mtu mwenye ghasia na
matukio ya utovu wa maadili.
Mapema siku ya Jumapili, chama cha wanamuziki wa Zambia
kilitoa taarifa na kutangaza kuwa wakati wa ziara ya Olomide nchini humo katika
kilele cha Mwaka Mpya wa 2013, alimpiga mtumbuizaji wake na mpiga picha mmoja
kwenye tamasha la muziki. Lakini alifanikiwa kuwatoroka polisi ambao walishindwa
kumkamata.
Kwa mujibu wa gazeti la Post la nchini Zambia, mwaka
2011, Olomide aliwatoroka polisi wa Zambia kwa kutumia pikipiki akiwa na
promota wake.
“Koffi ameonesha
kuwa ni mtu wa vurugu wakati wanamuziki wanatazamwa kama mabalozi wa amani,”
chama hicho kilisema.
Baada ya kufukuzwa nchini Kenya, Olomide, ambaye
anachukuliwa kama mwanamuziki mwenye nguvu zaidi katika wanamuzi wa sasa nchini
Kongo, alirudi nchini mwake na kukaribishwa kwa shamrashamra kwenye uwanja wa
ndege.
Nchini Togo, wanasheria wametoa wito wa kukamatwa na
kushitakiwa kwa Olomide baada ya kushindwa kutokea kwenye tamasha la muziki
mjini Lome ambapo alikuwa ameshalipwa sehemu ya pesa yake.
Nchini mwake taarifa za vyombo vya habari zinaonesha
kuwa amekuwa akihusishwa na matukio mbalimbali lakini uhusiano wake na serikali
ya Rais Kabila umekuwa ukimlinda dhidi
ya kufikishwa kotini.
Mnamo Oktoba 2014, alikamatwa na polisi nchini Kongo kwa
sababu ya kujipachika jina la Vieux Ebola (Ebola mzee), ambalo alilitumia
katika mabango yake kwa lengo la kutangaza tamasha lake la muziki.
Olomide alikamatwa katika kipindi ambacho ugonjwa wa
Ebola ulikuwa umeua watu 50 nchini humo na ambapo serikali ilikuwa ikipambana
dhidi ya madai ya kushindwa kushughulikia tatizo la ugonjwa huo. Serikali ilimwambia
kuwa jina hilo halikubaliki.
Mbali na jina hilo la Vieux Ebola, alikuwa na majina
mengine ya kujipachika yapatayo 35, rekodi ya majina ambayo hakuna mwanamuziki
yeyote duniani aliyeifikia.
Muda mfupi baada ya kukamatwa, alijipachika jina lingine
la “Benedict XVI wa Congo” — jambo lililowakasirisha waumini wengi wa
Kikatoliki kwa sababu jina hilo lilionekana kama ni tusi kwa Papa Benedict XVI,
kiongozi wa zamani wa Kanisa Katoliki duniani.
Mnamo Agosti 2012, alisimamishwa kwa muda wa miezi
mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kumshambulia prodyuza wake ambaye alikuwa
akimdai.
Mnamo Februari 15, 2012, hakimu mmoja wa Ufaransa alimtia
hatiani Olomide kwa makosa matatu ya ubakaji na vizuizi haramu, baada ya malalamiko
kutoka kwa waimbaji wake watatu.
Mwaka 2008, alikamatwa baada ya kumpiga mpiga picha
kwenye tamasha moja la muziki mjini Kinshasa. Baadaye ulifanyika usuluhishi.
Olomide ambaye majina yake mengine ni Antoine Christophe
Agbepa Mumba ni mwanamuziki maarufu, mtumbuizaji na prodyuza mwenye nyimbo
zinazovuma sana huku albamu zake zikiwa zimewekwa kwenye orodha ya kimataifa ya
albamu 1001 ambazo mtu anatakiwa kuzisikiliza kabla ya kufa.
CHANZO: The citizen
Kwa habari kupitia WhatsApp, jiunge: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment