BAADA ya ubashiri wa muda mrefu, Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana hatimaye ameandika barua ya kujiuzulu
ili kupisha Mwenyekiti mpya kupanga safu yake ya utendaji, imeelezwa.
Rais John Magufuli anatarajiwa kukabidhiwa kiti na Rais
mstaafu Jakaya Kikwete baada ya kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo katika
Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM utakaofanyika Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana,
Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, alisema suala hilo ni utamaduni uliojengeka
ndani ya chama hicho.
“Hili ni suala la utamaduni kwa sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya Taifa baada ya Mwenyekiti wa chama kupitishwa,” alisema Ole
Sendeka. “Ni utamaduni kwa sekretarieti kupisha na kumpa nafasi mwenyekiti mpya
wa chama kuunda safu yake ya utendaji ya chama.”
Alibainisha Kinana kwa niaba ya sekretarieti nzima
atakabidhi barua kwa mwenyekiti huyo ili yeye na sekretarieti hiyo waweze
kujihuzulu kumpisha Rais Magufuli kupanga safu yake.
Ili Rais Magufuli ateuliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM
ni lazima apate angalau asilimia 51 ya kura zitakazopigwa na Mkutano Mkuu
Maalumu huo, kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.
“Kama atapenda, amrejeshe atakayependa kumrejesha,
atakayetaka kufanya naye kazi kwa kadri itakavyompendeza... mwenyekiti mpya ataamua,”
alisema Ole Sendeka.
Alisema utamaduni huo hufanywa ili mwenyekiti aweze
kupata timu ya kufanya nayo kazi ambayo itakidhi matarajio yake, katika kuleta
maendeleo na mabadiliko ndani ya chama chenyewe.
Akizungumzia kuhusu taarifa zinazosambaa kwenye mitandao
ya kijamii kuwa Rais Magufuli atapigiwa kura ya hapana, Ole Sendeka alisema sio
za kweli.
Alisema Rais Magufuli hakuomba bali ni utaratibu wa
chama, na ndicho kinachompigia kampeni hivyo hakuna atakayemkataa kwa kuwa
wanachama ni waaminifu na watapiga kura ya ndio kumpigia Mwenyekiti wao mpya.
Rais Magufuli ambaye ni Rais wa tano aliyeapishwa
Novemba 5, 2015, atakuwa pia Mwenyekiti wa CCM wa tano.
Katika mkutano huo, chama hicho kimealika vyama vyote
vya siasa nchini, mabalozi, waasisi wa chama, vyombo vya habari na makundi mbalimbali
ya sanaa, alisema.
Utaratibu wa kuachiana kiti CCM ulianzia kwa Rais wa
Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alipomaliza muda wake mwaka 1995, na hivyo
kukabidhi nafasi ya Mwenyekiti kwa Benjamin Mkapa 1996 ambaye alifanya hivyo
pia kwa Kikwete mwaka 2006.
CHANZO: Nipashe
0 comments:
Post a Comment