
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UTEUZI WA WABUNGE KWENYE KAMATI
ZA KUDUMU ZA BUNGE
Katibu wa Bunge anatoa taarifa kwa umma kwamba:
(a) Kwa mujibu wa Kanuni ya 116 (3) ya Kanuni za Kudumu
za Bunge, Toleo la Aprili, 2013, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano amepewa
mamlaka ya kuteua Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa namna ambayo
itawezesha kila Mbunge kuwekwa kwenye Kamati mojawapo. Katika kufanya uteuzi
huo, Spika huzingatia vigezo mbalimbali vilivyoainishwa katika Kanuni ya 116
(5);
(b) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Job
Yustino Ndugai (MB), ametekeleza mamlaka yake ya uteuzi kwa mujibu wa Kanuni
tajwa hapo juu, kwa kuwateua kwanza Wabunge Kumi na Tano (15) kuwa Wajumbe wa
Kamati ya Kanuni za Bunge. Kamati hiyo imeundwa na kutangazwa kabla ya Kamati
zingine ili ifanye marekebisho ya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge
kuhusu majukumu ya Kamati zingine za Bunge kwa kuyashabihisha na majukumu ya
Serikali kwa kuzingatia Muundo wa Baraza la Mawaziri lililopo sasa. Lengo kuu
ni kuleta urahisi, ufanisi na tija kwa Bunge katika kuisimamia na kuishauri
Serikali;
(c) Kwa msingi huo, Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
ambayo Spika ndiye Mwenyekiti wake na Naibu Spika ni Makamu Mwenyekiti,
Kiongozi wa Upinzani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao ni Wajumbe kwa
nyadhifa zao itakutana katika Ofisi ya Bunge, Dar es Salaam siku ya Ijumaa
tarehe 15 Januari, 2016 saa tano kamili asubuhi katika Ukumbi wa Spika. Wajumbe
wengine ni: -
(i) Mhe. Makame Kassim Makame, MB. - Jimbo la Mwera;
(ii) Mhe. Tundu Antipas Mughwai Lissu, MB. - Jimbo la
Singida Mashariki;
(iii) Mhe. Jasson Samson Rweikiza, MB. - Jimbo la Bukoba
Vijijini;
(iv) Mhe. Ally Saleh Ally, MB. - Jimbo la Malindi;
(v) Mhe. Magdalena Hamis Sakaya, MB. - Jimbo la Kaliua;
(vi) Mhe. Salome Wycliff Makamba, MB. - Viti Maalum;
(vii) Mhe. Dkt. Jasmine Tiisekwa Bunga, MB. - Viti
Maalum;
(viii) Mhe. Zainab Athman Katimba, MB. - Viti Maalum;
(ix) Mhe. Balozi Adadi Mohamed Rajab, MB. - Jimbo la
Muheza;
(x)Mhe. Dkt. Charles John Tizeba, MB. - Jimbo la
Buchosa; na
(xi) Mhe. Kangi Alphaxard Lugola, MB. - Jimbo la
Mwibara.
(d) Spika atakamilisha uteuzi wa Wajumbe katika Kamati
zingine za Bunge kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Pili wa Bunge tarehe 26
Januari, 2016, Mjini Dodoma ili kutoa fursa kwa Kamati zote kuchagua Viongozi
wake na kuandaa Mpango Kazi kwa mwaka 2016/17; na
(e) Wabunge wote wanatangaziwa kuwa wawe wamefika Dodoma
tarehe 20 Januari, 2016 tayari kwa kuanza kwa Kamati za Bunge na Mkutano wa
Bunge, isipokuwa Kamati ya Wabunge (Caucus) wote wa Chama cha Mapinduzi
wanatakiwa kuwa Mjini Dodoma tarehe 17 Januari, 2016 kwa Mkutano wao.
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
Ofisi ya Bunge,
S. L. P. 9133,
DAR ES SALAAM.
11 Januari, 2016.
0 comments:
Post a Comment