Mwalimu wa Shule ya Msingi Peramiho, Songea mkoani
Ruvuma, Baraka Mwakajila (29), amekutwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa
kutumia shati ndani ya nyumba alimokuwa akiishi.
Kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Resocatus
Malimi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea juzi saa sita mchana katika mji
mdogo wa Peramiho, nje kidogo ya Manispaa ya Songea.
Malimi alisema inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, Mwalimu
Mkuu Msaidizi, Rashid Pilly, aligundua kujinyonga kwa mwalimu huyo, baada ya
kupita eneo la nyumba aliyokuwa anaishi na kuona nzi wengi wametapakaa kwenye
eneo la dirisha la chumba alichokuwa analala.
Alifafanua zaidi kuwa Mwalimu Pilly baada ya kuona hali
hiyo, alisogea hadi mlangoni na kukuta mlango ukiwa umefungwa huku eneo hilo
likiwa na harufu kali iliyoashiria kuna kitu ambacho kimeoza.
Alisema baadaye Mwalimu Pilly alilazimika kwenda kutoa
taarifa kwenye kituo kidogo cha Polisi cha Peramiho na baadaye askari polisi
wakiwa wameongozana na mganga, walifika eneo la tukio.
Baada ya kufika alisema walivunja mlango na kuingia
ndani ya nyumba hiyo ambako walimkuta Mwalimu Mwakajila akiwa tayari ameshakufa
muda mrefu baada ya kujinyonga.
Alisema Mwakajila alijinyonga ndani ya nyumba ambayo ni
mali ya shule na askari walikuta barua chini ya sehemu aliyojinyongea ilikuwa
imeandikwa Januari 4 mwaka huu na mwanamke (jina linahifadhiwa), anayedaiwa
kuwa ni mpenzi wake, ambaye alimtaka aachane naye na aendelee na maisha yake.
Malimi alisema polisi baada ya kuiona na kuisoma,
waliendelea kufanya upekuzi mwili wa marehemu na kukuta karatasi kwenye mfuko
wa suruali yake, ambapo Mwakajila aliandika Januari 2 mwaka huu, akimtuhumu
mpenzi wake huyo kuwa amekuwa malaya na mlevi.
Kamanda Malimi alisema polisi wanaendelea na uchunguzi
zaidi kuhusiana na tukio hilo na mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu kwa
ajili ya taratibu za mazishi.
0 comments:
Post a Comment