
Milipuko miwili ya mabomu imeutikisa mji mkuu wa Indonesia,
Jakarta, huku ripoti zikisema kuwa kwa uchache watu wanne wamepoteza maisha.
"Watu wanne wamekufa, polisi mmoja na raia watatu,”
shirika la habari la AFP limemnukuu msemaji wa polisi nchini humo, Anton
Charliyan, akisema.
Kwa mujibu wa akaunti rasmi ya polisi kwenye mtandao wa Twitter,
mlipuko mmoja umetokea karibu na eneo la biashara liitwalo Sarinah mall.
Ufyatuaji wa risasi ulisikika baada ya mlipuko wa
asubuhi katika eneo hilo ambalo pia lina hoteli za kifahari, balozi na ofisi
mbalimbali.
Charliyan amesema milio ya risasi imekoma lakini
washambuliaji bado hawajakamatwa, na polisi wana wasiwasi kuwa kutakuwa na
milio zaidi ya risasi.
Mashuhuda walionukuliwa na shirika la habari la Associated
Press, wamesema kuwa mlipuko huo ulisababishwa na bomu, lakini hakukuwa na
uthibitisho wa haraka wa madai hayo.
Kituo kimoja cha televisheni kutoka nchini humo kimesema
kuwa jumla ya milipuko sita ilisikika.
Hakukuwa na maelezo ya haraka kuhusu wahusika wa
mashambulizi hayo.
Indonesia imekuwa kwenye tahadhari kufuatia vitisho vya
makundi ya wanamgambo huku polisi wakianzisha msako na operesheni dhidi ya watu
wanaoshukiwa kuwa na mafungamano na makundi yenye siasa kali.
Wakati wa kilele cha Mwaka Mpya kiasi cha polisi na
askari 150,000 walipelekwa kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya makanisa, viwanja
vya ndege na maeneo mengine ya umma.
Pia zaidi ya polisi 9,000 walipelekwa mjini Bali, eneo
ambalo lilitokea shambulizi baya la kigaini lililoua watu 202 mwaka 2002.












0 comments:
Post a Comment