![]() |
| Moshi mkubwa ukionekana ndani ya jengo la ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran baada ya waandamanaji wenye hasira kuuvamia mapema Jumapili. |
Qatar imekuwa nchi ya karibuni kabisa kuiunga mkono Saudi Arabia katika mgogoro wake na Iran, na kuchukua hatua za kumuita nyumbani balozi wake wa Tehran kama radiamali dhidi ya mashambulizi yaliyofanywa na waandamanaji dhidi ya ubalozi wa Saudia mjini Tehran wiki iliyopita.
Jordan, Djibouti, na Uturuki zimeelezea kuiunga mkono
Saudi Arabia dhidi ya kitendo cha kushambuliwa ubalozi wake kufuatia kunyongwa
kwa kiongozi maarifu wa kishia katika taifa hilo linaloongozwa na Wasunni.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema kuwa kunyongwa
kwa watu 47 kwa makosa ya ugaidi nchini Saudi Arabia lilikuwa suala la “ndani”.
Miongoni mwa walionyongwa ni sheikh wa kishia, Nimr al-Nimr – hatua iliyoibua
ghadhabu za kimadhehebu katika ukanda huo.
"Watu arobaini na sita kati ya walionyongwa ni
Wasunni na walinyongwa kwa sababu walikuwa na uhusiano na al-Qaeda. Mmoja wao
alikuwa kiongozi wa kidini wa kishia. Uamuzi huu ulichukuliwa mapema na Saudi
Arabia ikautekeleza. Huu ni uamuzi wao,” Erdogan alisema katika hotuba yake
katika mji mkuu wa Uturuki, Ankara.
Aidha, Rais huyo alisema kuwa wale walionyamazia vifo
vya watu katika vita vya Syria wanalalama kwa kunyongwa mtu mmoja nchini Saudi
Arabia, akionekana kuisema Iran ingawa hakutaja majina.
"Mnaunga mkono [utawala
wa Syria] kwa siri au kwa dhahiri. Mnatoa msaada wa kifedha na silaha kwa
muuaji [Rais Bashar] Assad," Erdogan alisema. "Ubalozi wa Saudi
Arabian embassy [nchini Iran] ulishambuliwa kwa mabomu. Ubalozi wake nchini
Iraq pia ulihujumiwa. Hili jambo halikubaliki katika uhusiano wa kimataifa.”
Wakati huo huo, Rais
wa Iran, Hassan Rouhani, aliitaka mahakama nchini humo kuwachukulia hatua
haraka sana wale walioushambulia ubalozi wa Saudia.
"Kwa kuwaadhibu
washambuliaji na wale waliochochea uhalifu huu wa wazi, tutapaswa kukomesha
moja kwa moja hasara hiyo na matusi hayo dhidi ya heshima ya Iran na usalama wa
taifa,” Rais Rouhani alinukuliwa akisema katika barua iliyochapishwa na shirika
la habari nchini humo la IRNA.
Nayo Djibouti imekata
uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran katika kupinga kitendo cha kushambuliwa
ubalozi wa Saudi Arabia. Nchi hiyo imeungana na Saudi Arabia, Bahrain na Sudan katika
kukata kabisa uhusiano na Iran.
"Djibouti imekata
uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran katika kuonesha mshikamano na Saudi
Arabia," Waziri wa Mambo ya Nje, Mahamoud Ali Youssouf, ameliambia shirika
la habari la Reuters kwa ujumbe wa maandishi.
Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait zimewaita mabalozi
wao walioko Iran.
Wakati huo huo, Jordan imemuita balozi wa Iran mjini Amman na
kulaani shambulizi dhidi ya ubalozi huo, na “uingiliaji kati wa Iran” katika
mambo ya Waarabu, shirika la habari la Jordan Petra, limesema.
Waandamanaji
wa Kiiran waliuvamia ubalozi wa Saudia na majengo mengine ya kidiplomasia siku
ya Jumapili. Tangu kutokea kwa mashambulizi hayo, Iran inasema kuwa
imewakamata washambuliaji hao na kulaani ghasia hizo.

0 comments:
Post a Comment