VIJANA tisa wenye vipato vya kawaida kutoka maeneo
mbalimbali nchini, wametimiza ndoto ya umoja ni nguvu kwa kuanzisha kampuni ya
kizalendo wanayotaka iongoze nchini kwa uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na
misitu zitakazo zingatia ubora wa kimataifa.
Vijana hao German Ibreck, Anael Samuel, Prosper Moshi,
Edward Masuzya, Edwin John, Baraka Maduhu, Leevan Maro, Beatrice Masalu na
Elisha Msengi wameanzisha kampuni ijulikanayo kama Agora Wood Products Ltd.
Kampuni hiyo iko katika hatua za awali za ujenzi wa
kiwanda cha kutibu nguzo za umeme na bidhaa zingine zifananazo na hizo katika
kijiji cha Igwachanya, kata ya Mseke, wilayani Iringa.
Jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda hicho kitakachokuwa
na uwezo wa kutibu wastani wa nguzo za umeme 200 kwa siku, liliwekwa juzi na
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hafla iliyohudhuriwa na wananchi
wa kijiji hicho, na viongozi wa serikali ya mkoa na wilaya ya Iringa.
Afisa Mtendaji wa kampuni hiyo, Elisha Msengi alisema
kiwanda hicho kitatumia teknolojia mpya katika kuwezesha dawa kupenya vizuri
ndani ya nguzo na bidhaa zingine zitokanazo na miti na hivyo kuongeza ubora na
matumizi ya muda mrefu ya bidhaa hizo.
“Kitakapokamilika, kiwanda kitatoa ajira za moja kwa
moja zaidi ya 50 na nyingine 200 zisizo za moja kwa moja,” alisema na kuongeza
kwamba kiwanda hicho kitachangia kwa kiwango kikubwa mapato ya fedha za
halmashauri na serikali kuu kwa njia ya kodi na tozo muhimu.
Alisema ujenzi wa majengo na miundombinu iliyopo katika
kiwanda hicho ulianza Septemba, 2015 ukihusisha ununuzi wa mitambo, ardhi,
malighafi za ujenzi na kazi kwa zaidi ya Sh Milioni 500 ambazo zimechangwa na
vijana hao.
Alisema hadi kukamilika kwake, kiwanda hicho kitagharimu
zaidi ya Sh Bilioni 2.5 na akashangaa mradi huo wenye manufaa makubwa kwa mkoa
na Taifa ulivyokosa mkopo kutoka katika moja ya benki za hapa nchini pamoja na
kusubiri kwa miezi tisa tangu mkopo huo uombwe.
Akiweka jiwe la msingi katika kiwanda hicho, Mkuu wa
Mkoa wa Iringa alisema; “natiwa moyo na kufurahishwa sana kuona kwamba kiwanda
hiki kimejengwa na kumilikiwa na wazawa kwa asilimia 100.”
Masenza alisema serikali ya awamu ya tano ya Dk John
Magufuli imelenga kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda ili badala
ya kuuza malighafi, ziuzwe bidhaa ambazo zimetengenezwa kwa ubora na zenye
thamani katika soko la ndani na nje.
Alisema ili kufikia lengo hilo serikali hiyo imedhamiria
kuondoa ukiritimba ambao umekuwa ukikatisha tamaa wawekezaji wa ndani na nje
wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya viwanda.
Ili kianze kufanya kazi kiwanda hicho ambacho mitambo
yake ya kutibu bidhaa hizo za miti inaendelea kufungwa, kinahitaji kuunganishwa
na umeme wa njia tatu na transfoma na ujenzi wa barabara ya mtaa kuelekea
kiwandani.
“Tunawakaribisha Tanesco washirikiane nasi kupitia
mpango wa Public Private Partnership, kifedha, kiutaalamu na kiushauri katika
kuzalisha nguzo bora za umeme,” alisema Afisa Mtendaji wa kampuni hiyo.
CHANZO: Wavuti.com
0 comments:
Post a Comment