![]() |
| Neymar anaweza kuwa mtu sahihi kwa Man United – lakini bosi wa Barca Luis Enrique jana usiku alikataa kulizungumzia hilo. |
Tetesi zilianza kuibuka wiki iliyopita kuhusu uwezekano
wa nyota Mbrazil, Neymar, kuhamia kalabu ya Manchester United.
Mshambuliaji huyo hakuonekana katika mechi ya ufunguzi
wa ligi ya Hispania, maarufu kama La Liga, ambapo klabu yake iliibuka na
ushindi wa 1-0 dhidi ya Athletic Bilbao, huku staa wa zamani wa Liverpool Luis
Suarez akipachika bao pekee katika mchezo huo.
Hata hivyo, suala la kutoonekana dimbani halikutiliwa
shaka kwa sababu ndio kwanza amerudi mazoezini baada ya kupona majeraha.
Lakini tetesi zinaendelea kuvuma kwa kasi kuwa Neymar anaweza
kuhama kipindi hiki cha majira ya joto, huku United wakihusishwa na dili hilo.
KOCHA AKWEPA KULIZUNGUMZIA
Jana bosi wa Barcelona Luis Enrique alikataa kuzungumzia
tetesi hizo, akisema: “Hainipendezi kuzungumzia tetesi, wala habari za aina
hii. Ninachotaka tu ni kumakinika kwenye kile kinachotokea katika timu yangu.”
MAZUNGUMZO
Gazeti la The Guardian linadai kuwa nyota huyo mwenye
umri wa miaka 23 anafanya mazungumzo na Manchester United, jambo ambalo linaweza
kuonekana kuwa la kushangaza kwa wakati huu. Kuna mitazamo kadhaa kuhusu jambo
hili na miongoni mwa mitazamo hiyo ni kwamba tetesi hizi zinaweza kuilazimisha Barcelona
kumuongezea mshahara.
Mtazamo mwingine ni kwamba anaweza kuwa ameahidiwa kitita
kikubwa zaidi na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza. Hata hivyo, yumkini kuna
sababu nyingine inayomfanya kuchukua hatua hiyo.
NAFASI
Kwa timu nyingi duniani Neymar anaweza kuwa mchezaji
tegemeo. Mchezaji huyo angependa kupewa nafasi kubwa kama anavyopewa katika
timu yake ya taifa la Brazil. Lakini, katika klabu ya Barcelona mambo ni
tofauti, kwa sababu kila mara Lionel Messi amekuwa akichukua nafasi yake.
Ni ngumu kuhoji ubora wa Messi kwenye michuano ya Klabu
Bingwa ya Ulaya. Ni miongoni mwa wachezaji bora kuwahi kushuhudiwa katika
michuano hiyo. Neymar alijikuta katika wakati mgumu kushindania namba na mkali
hiyo pale Nou Camp.
Hata hivyo, msimu uliopita alionekana kuikubali hadhi ya
Messi na ghafla akapata nafasi, akafunga mabao 32 katika mashindano yote na
kusaidia mabao 7. Alitengeneza mchanganyiko machachari pamoja na Messi na Luis
Suarez.
Watatu hao wanaaminika kuwa na uhusiano mzuri hata nje
ya dimba, hivyo yumkini Neymar ametambua kuwa hakuna umuhimu wa kugombania
nafasi ya juu katika klabu ya Barcelona.
Hata hivyo Neymar sio mtu mdogo klabuni, lakini hawezi
kuchukua nafasi ya Lionel Messi na hilo linaweza kuongeza mashaka ya Mbrazil
huyo kuhusu mustakbali wake klabuni.
Klabu ya Manchester United inapiga hatua kubwa chini ya
kocha mkongwe Louis van Gaal na wanaonekana kuwa ndani ya misimu michache ijayo,
kama si msimu huu, watarudi kuwa miongoni mwa vigogo wa Ligi Kuu.
Kama atahamia huko, basi atakuwa amefanya chaguo zuri
litakaloweza kumhakikisha nafasi na hadhi kubwa dimbani.

0 comments:
Post a Comment