
Ndege moja ya Indonesia iliyobeba abiria 54 imepoteza
mawasiliano na chumba cha kuongozea ndege katika jimbo la Papua nchini
Indonesia.
Kwa mujibu wa ripoti za awali, ndege hiyo ni ndege ya
shirika la ndege la Trigana Air ATR 42, na imepoteza mawasiliano baada ya
kuondoka katika uwanja wa ndege wa mji mkuu wa jimbo hilo, Jayapura na ilikuwa ikijiandaa kutua katika wilaya ya Oksibil yenye milima mingi.
Kwa mujibu wa mkurugenzi wa operesheni wa shirika hilo,
Beni Sumaryanto, ndege hiyo iliwasiliana na chumba cha kuongozea ndege katika
uwanja wa ndege wa Oksibil dakika kumi kabla ya kutua na kuomba kutua. Lakini,
ndege hiyo haikuwasili.
Shirika la Trigana lilituma ndege nyingine kwenda
kuitafuta, lakini nayo ililazimika kurudi kutoka na hali mbaya ya hewa katika
eneo hilo ambalo linajulikana kuwa na hali ya hewa isiyotabirika.
Ndege hiyo ilikuwa imebeba watu wazima 44, watoto 5, na
wafanyakazi 5.
Japokuwa wizara ya Uchukuzi ya Indonesia imesema kuwa
sababu ya kutoweka kwa ndege hiyo haijulikani, Sumaryanto anasema kuwa hali
mbaya ya hewa inaweza kuwa imechangia kupotea kwa ndege hiyo.
Wiki iliyopita, ndege moja ya shirika la ndege la Komala
Air la nchini Indonesia, ilipata ajali katika wilaya ya Yahukimo katika jimbo
la Papua, iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na wengine watano kujeruhiwa vibaya
sana. Ajali hiyo ilisemekana kusababishwa na hali mbaya ya hewa.
Katika miezi ya hivi karibuni, Indonesia imekumbwa na
jinamizi la usalama mdogo wa usafiri wake wa anga.
Mwezi Desemba mwaka jana, ndege ya shirika la ndege
la AirAsia iliyokuwa ikisafiri kutoka
mji wa Surabaya nchini humo kwenye Singapore ilipata ajali katika Bahari ya
Java kutokana na hali mbaya ya hewa na kusababisha vifo vya watu wote 162
waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
0 comments:
Post a Comment