![]() |
| Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Samson Mwigamba akionesha mkoba wenye fomu za urais alizomchukuliwa Profesa Kitila Mkumbo katika ofisi za NEC Dar es Salaam jana. |
Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) hakina unahika iwapo kitamsimamisha mgombea wa Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 baada ya wagombea kiliowawasilisha katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukataa kubeba jukumu hilo.
Jana
asubuhi, katibu mkuu wa chama hicho general Samson Mwigamba aliwachukulia fomu
za uteuzi Profesa Kitila Mkumbo na mgombea wake mwenza Bi. Hawra Shamte lakini kwa mshangao walijiweka
mbali na hatua hiyo.
Awali
bwana Mwigamba aliwaambia waandishi wa habari kuwa Profesa Kitila Mkumbo na Bi
Hawra Shamte wameteuliwa na Kamati Kuu ya chama kuwa wagombea wake.
Hata
hivyo, alisema kuwa chama chake kilikuwa kikishauriana na Profesa Mkumbo kukiwakilisha katika uchaguzi wa Oktoba
25 akielezea matumaini na matarajio kuwa hatalikataa pendekezo lao.
Lakini
katika hali ya sintofahamu, Profesa Mkumbo aliandika katika mitandao ya kijamii
kuelezea wazi kuwa hatagombea urais kupitia chama hicho.
“Nimekuwa
nikilitafakari jambo hili tangu Alhamisi nilipoombwa rasmi kutafakari uwezekano
wa mimi kugombea baada ya juhudi zetu za kutafuta mgombea kushindikana.
Nimefanya mawasiliano mapana katika familia, ndani ya chama, chuoni
ninapofanyia kazi, Kanisani kwangu,na kwa watu na taasisi mbalimbali ninazohusiana
nazo,” aliandika katika ukurasa wake wa Facebook na kuongeza kuwa:
“Baada
ya tafakari na mawasiliano (consultations) mapana nasikitika kusema kwamba sina
utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia, na kisiasa
kuniwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huu.”
Profesa
Mkumbo, ambaye ni mhadhiri wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
mkuu wa sera na utafiti wa chama cha ACT-Wazalendo alikiri kuwa amewaangusha
wanachama kwa uamuzi wake huo lakini akawaomba viongozi wengine waandamizi wa
chama hicho kukiwakilisha katika kinyang’anyiro cha urais. Baadaye, Profesa
Mkumbo alisema kuwa ana uhakika chama chake kitaendana na muda uliowekwa na NEC
kuwasilisha majina ya wagombea wanaofaa.
Kwa
upande wa Bi Hawra Shamte mambo yalionekana kuwa yenye kuchanganya zaidi. Mwigamba
alipoulizwa kwenye ofisi za NEC iwapo jina husika ni la mhariri mwandamizi wa
kampuni ya Mwananchi Communications Limited, alikanusha huku akisisitiza kuwa
watu wasubiri kumuona mgombea mwenza wakati wa urejeshaji wa fomu siku ya
Ijumaa wiki hii.
Naye
Bi Hawra Shamte alipoulizwa alisema: “Yawezekanaje mtu aniwakilishe wakati nipo
na nina uwezo wa kufanya hivyo mimi mwenyewe?” aling’aka.
“Muda
huu ninapozungumza sijui chochote kuhusu ushiriki wangu katika uchaguzi ujao
kama mgombea na wala sina hata uanachama wa chama chenyewe,” aliongeza.
Haya
yanatokea wakati zimebaki siku tatu pekee kwa wagombea kuchukua na kurudisha
fomu katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Vyama
vya siasa vinatarajiwa kuzindua rasmi kampeni zao Jumamosi wiki hii. Kampeni hizo
zitahusisha nafasi za udiwani, ubunge na urais.
Mpaka
sasa haijulikani iwapo ACT-Wazalendo kitashiriki uchaguzi bila mgombea urais.
Jana,
kundi wa wanachama wa chama hicho walifika makao makuu ya chama wakiwa na
mabango yaliyomtaka Profesa Mkumbo kugombea urais.

0 comments:
Post a Comment