
Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema hana
mpango na hafikirii tena kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili
nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam jana, Dk Salim alisema alipowania nafasi
hiyo mwaka 2005, hakuwa na ufahamu mzuri kuhusu mchakato huo lakini baadaye
alibaini kwamba, mbali na rekodi ya utendaji, kuna mambo mengine yanayohitajika
katika kinyang’anyiro hicho na kwamba hata watu wanaomfikiria na kutaja jina
lake miongoni mwa wanaoweza kuwania tena nafasi hiyo, wanakosea.
“Sifikirii tena, hii ni zamu ya kizazi kingine. Ila
nitaendelea kuisaidia nchi yangu katika nyanja mbalimbali kadri ya uwezo
wangu,” alisema.
Dk Salim ambaye mbali na uwaziri mkuu amewahi kushika
nafasi nyingine mbalimbali kitaifa na kimataifa, alisema uzoefu alioupata
katika kinyang’anyiro cha urais unatosha.
Alipoulizwa kama uzoefu huo ni mbaya au mzuri kwake,
alisema ni mchanganyiko.
Dk Salim aliwahi kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa (UN) na kushindwa kutokana na
kura ya veto ya Marekani, pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa
Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU). Pia aliwahi kuwa Rais wa
Bunge Kuu la UN mwaka 1979 na 1980.
Licha ya kujitokeza mara moja kuomba uteuzi wa CCM
kuwania urais 2005, nyota yake katika nafasi hiyo ilianza kuwaka tangu mwaka
1985 akiwa Waziri Mkuu pale aliposhindanishwa katika Kamati Kuu ya CCM na
aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa pamoja aliyekuwa Makamu wa Rais wakati
huo, Ali Hassan Mwinyi ambaye alipitishwa kiitifaki na kushinda kiti hicho.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Makamu
mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisimulia jinsi Mwinyi alivyopita, kwa
sababu alikuwa Makamu wa Rais, hivyo wajumbe wa Kamati Kuu walikosa hoja na
sababu za kumwacha na kumchukua Waziri Mkuu aliyekuwa chini yake kiitifaki.
“Makamu wa Rais ukimruka maana yake hatoshi, wakaona
hawana maelezo hayo, ikabidi wamteue Mwinyi,” alisema Msekwa.
SIFA ZA VIONGOZI
Katika hatua nyingine, Dk Salim alisema kuna umuhimu
mkubwa wa kuandaa viongozi hasa mtu anayekwenda kushika nafasi ya urais
atakayekwenda sambamba na mahitaji ya kizazi cha sasa alichokiita cha ‘dot
com’.
“Hapa sizungumzii viongozi wa CCM au wa Chadema au chama
kingine, nazungumzia viongozi wa nchi watakaoweza kufanyia kazi matatizo ya
Watanzania.
“Ni vizuri viongozi wakaandaliwa, isiwe mtu anaibuka tu
anagawa hela halafu anashinda. Anatakiwa mtu atakayeweza kushughulikia matatizo
hayo. Watanzania ni wapole na wavumilivu lakini wanazungumza. Hivyo anahitajika
kiongozi atakayesikiliza mahitaji yao na kutoa suluhisho, si kutoa ahadi za
uongo,” alisema. Dk Salim alisema katika kipindi hiki, anahitajika kiongozi
atakayekuwa juu ya tofauti za kisiasa, kidini, asili.
“Unajua hapa nchini kama ilivyo mahali pengine,
ukiingiza mgawanyiko wa kidini wakati familia nyingi zina watu wa dini tofauti,
wote wataathirika.”
VIONGOZI NA RUSHWA
Akizungumzia tatizo la rushwa, Dk Salim alisema ni kubwa
na kadri linavyoongezeka, linakuwa adui wa uwajibikaji, demokrasia.
Alisema katika enzi za utumishi wake nje ya nchi,
alikuwa akiona rushwa ilivyokithiri katika nchi mbalimbali, lakini hapa
nyumbani pakiwa salama hadi akawa anasema Tanzania ina bahati, kauli ambayo
hawezi kuisema sasa.
Dk Salim alibainisha kuwa uongozi unaoingia madarakani
kwa rushwa hauwezi kuwa mzuri kwa nchi na athari zake zinaonekana hadi ngazi ya
chini katika huduma za jamii kama mahakamani, polisi na hospitalini.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment