Polisi wakijaribu kuudhibiti umati wa watu kwenye eneo la tukio la milipuko ya mabomu iliyogharimu maisha ya watu 10 Mei 16, 2014. |
Kwa uchache watu 10 wamepoteza maisha na zaidi ya 70
kujeruhiwa baada ya kutokea milipuko miwili kwenye soko la Gikomba mjini
Nairobi.
Polisi wanasema kuwa mlipuko mmoja ulipiga gari moja ya
abiria aina ya daladala, huku bomu la pili likilipuka ndani ya soko hilo.
Kwa mujibu wa mkuu wa polisi wa jiji la Nairobi, Benson
Kibue, mtuhumiwa mmoja amekamatwa kuhusiana na shambulizi hilo.
Naye msemaji wa Hospitali Kuu ya Kenyatta National
Hospital, Simon Ithae, amesema kuwa kwa
uchache watu 70 wamejeruhiwa katika tukio hilo, wengi wao wako katika hali
mbaya,
Miji ya Nairobi na Mombasa imekuwa ikikumbwa na
mfululizo wa milipuko tangu Septemba mwaka jana.
Mnamo Aprili 13, watu wanne, wakiwemo polisi wawili,
walipoteza maisha katika mlipuko wa bomu lililotegwa kwenye gari nje ya kituo kimoja
cha polisi mjini Nairobi.
Mwezi Septemba mwaka jana, shambulizi lililofanywa
kwenye jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi liliwaua watu wasiopungua
67.
Wapiganaji wa kundi la Al-Shabab kutoka Somalia wamekuwa
wakitupiwa lawama za mashambulizi hayo.
Wanamgambo hao walisema kuwa shambulizi la westgate ni
radiamali dhidi ya uwepo wa jeshi la Kenya nchini Somalia. Askari wa Kenya
pamoja na wengine kutoka nchi za Unagda Burundi, Djibouti, Sierra Leone na Ethiopia
ni sehemu ya Kikosi cha Umoja wa Afrika nchini humo (AMISOM).
0 comments:
Post a Comment