MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu Kiwanda cha Kutengeza Dawa (TPI Ltd) Ramadhani Madabida na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka matano ya usambazaji wa Dawa feki za kurefusha maisha kwa waathirika wa Ukimwi na kuisababishia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hasara ya zaidi ya Sh.milioni 148.3.
Mbali na Madabida washtakiwa wengine ni, Meneja
Uendeshaji Seif Shamte, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Mkoa
wa Dar es Salaam na Meneja Masoko, Simon Msoffe, Mhasibu Msaidizi Fatma Shango,
Sadiki Materu na Evans Mwemezi.
Walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulila
Mwaseba aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo ya Uhujumu uchumi namba 5 ya mwaka 2014,
ilifikishwa jana katika viunga vya mahakama hiyo saa 3:13 asubuhi huku
washtakiwa wakiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu wa jeshi la polisi na
kuhifadhiwa kwenye chumba cha mahabusu ya mahakama kabla ya kupandishwa
kizimbani.
Kimaro aliudai kuwa shitaka la kwanza linamkabili
mshitakiwa Madabida, Shamte, Msoffe, na Shango, wanadaiwa kwamba Aprili 5 ,2011
jijini Dar es Salaam waliuza na kuisambazia Idara ya Bohari Kuu ya Madawa
makopo 7776 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral ambazo zinajumuisha gramu 30
za Stavudine,gramu 200 za Verirapine na Batch namba OC 01.85 zikionesha
zimezalishwa Machi 2011 na kuisha muda wake Februari 2013 kwa lengo la kuonesha
ni dawa halisi aina ya Antiretroviral wakati wakijua si kweli.
Shitaka la pili pia la usambazaji wa dawa hizo ambalo
linawakabili washtakiwa hao wane ambapo wanadaiwa kwamba,wakiwa na nyadhifa zao
hizo,waliisambazia Bohari kuu ya madawa kopo 4476 za dawa aina ya
Antiretroviral ambazo zinajumuisha gramu 30 za Stavudide,gramu 200 za
Nevirapine na gramu 150 za Lamivudine zenye batch namba OC 01.85 zikionesha
zimezalishwa Machi 2011 na kuisha muda wake Februari 2013 kwa lengo la kuonesha
ni dawa halisi aina ya Antiretroviral wakati wakijua si kweli. Katika shitaka
la tatu washitakiwa hao pia wanadaiwa kwamba Kati ya Aprili 12 hadi 29 ,2011
jijini Dar es Salaam wakiwa na nia ya kudanganya kwa pamoja walijipatia
Sh.148,350,156.48 kutoka Kitengo cha Bohari Kuu ya Madawa baada ya kudanganya
kwamba fedha hizo ni malipo ya dawa halisi aina ya Antiretroviral wakati
wakijua si kweli.
Kimaro aliendelea kudai katika shitaka la nne
linamkabili Sadick na Evans ambao wanadaiwa kwamba,katika tarehe tofauti kati
ya Aprili n5 na 13 mwaka 2011,jijini Dar es Salaam wakiwa kama waajiriwa wa
Idara ya Bohari Kuu ya Madawa kama Meneja udhiditi Ubora na Ofisa udhibiti
ubora ,huku wakijua nia ya kutendeka kwa kosa ambalo ni kusambaza dawa
bandia,walishindwa kutumia nyadhifa zao kudhibiti kosa hilo lisitendeke.
Shitaka la tano,linawakabili washitakiwa wote ambao
wanadaiwa kwamba kati ya Aprili 5 hadi 30,2011, kwa nafasi zao na kutotekeleza
majukumu yao ipasavyo waliisababishia bohari Kuu ya Madawa kusambaziwa dawa
hizo bandia na hivyo Bohari kupata hasara ya Sh. 148,350,156.48 . Baada ya
kusomewa mashitaka hayo,washtakiwa wote walikana tuhuma hizo na upande wa
Jamhuri ulidai kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Pia, upande wa Jamhuri ulidai kwamba hauna pingamizi na
dhamana kwa washtakiwa wote. Hakimu Mwaseba alisema washtakiwa watakuwa nje kwa
dhamana kama watakuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakatoa fedha taslimu
Sh.12,365,513 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha kwa
kila mshitakiwa.
Hata hivyo, ni washtakiwa wawili tu -wa kwanza na wa
tano Madabida na Materu - walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana huku
wengine walipelekwa mahabusu hadi Februari 24, mwaka huu kesi yao itakapotajwa.

0 comments:
Post a Comment