
ISO 9001: 2008 CERTIFIED
TAARIFA KWA UMMA
Mamlaka ya
Mapato Tanzania inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania na wafanyabiashara kwa
ujumla Kuwa inasikitishwa na mgomo wa wafanyabishara kwa kufunga maduka
maeneo mbali mbali nchini.
Ifahamike kuwa
Matumizi ya mashine ya EFD ni jambo la kisheria na lilipitishwa na bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2011.
Pamoja na sheria
kupitishwa, viongozi wakuu wa nchi walikwisha litolea tamko kwa nyakati tofauti
kwa kuanzia na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mwezi wa Machi 2011.
Pia Makamu wa
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohammed Gharib Billal alikazia
jambo hili tarehe 8 Mwezi November mwaka 2013.
Waziri mkuu wa
Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mhe. Mizengo Peter Pinda alilitolea tamko pia
Mwezi Desemba 2013 wakati akiahirisha Bunge kwa kusisitiza msimamo wa
serikali kwa utekelezaji wa kisheria wa matumizi wa mashine za EFD.
Tarehe 29 Janauri
2014, Waziri wa Fedha Mhe Saada Mkuya Salum aliweka bayana msimamo wa Serikali
kwa kusisitiza kuwa Matumizi ya mashine za EFD ni swala la kisheria na
litaendelea kutekelezwa kwa mujibu wa sheria akisisitiza kuwa muda wa mwisho wa
nyongeza kwa wafanyabishara kununua mashine ilikuwa ni Tarehe 31 Januari 2014
baada ya kuongeza muda mara tatu kwa nyakati tofuati.
Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) pia kwa nyakati tofauti na maeneo tofuati imelitolea tamko
jambo hili na itaendelea kufanya hivyo.
Kwa masuala ya
kiutendaji yaliyolalamikiwa yamefanyiwa kazi na yanaendelea
kufanyiwa kazi ikiwemo utoaji wa Elimu kwa umma.
Mamlaka ya Mapato
Tanzania inapenda kuwafahamisha wafanyabiashara na umma kwa ujumla kuwa
watu wanaolazimisha wafanyabishara wenzao kufunga maduka kwa kuwatishia na
kuwashurutisha wanavunja sheria kwa kusababisha uvunjifu wa amani nchini
na hivyo mkono wa sheria utawafikia. Pia imefahamika kuwa baadhi ya watu
wanaoshurutishwa kufunga biashara sio walengwa bali hutumika kuhalalisha azma
ya wale wenye nia mbaya
TRA imekuwa
ikipokea taarifa na maombi kutoka kwa baadhi ya wafanyabishara na wananchi wema
wakiomba ulinzi ili wafungue maduka yao na kufanya biashara maana ndio ajira
yao na mahali pakujipatia riziki ya kila siku.
Ifahamike kwamba
wale wote wanaoshinikiza na kulazimisha wenzao kugoma wanavunja sheria kwa
kuwalazimisha wafanyabiashara kugomea agizo halali la kisheria hivyo kwa wale
wote wanaotishiwa au kushurutiswa watoe taarifa kwa kupiga simu namba
zifuatazo 0786 800 000, 0713 800333, 0800 110016 au barua pepe info@tra.go.tz
“PAMOJA TUNAJENGA TAIFA LETU”
IMETOLEWA NA KAIMU KAMISHNA MKUU
MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA
0 comments:
Post a Comment