
KIONGOZI kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni, Mh. Freeman Mbowe, ametahadharisha dhidi ya
wanasiasa wanaoitaka serikali kujiondoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza katika Mkutano wa 13 wa Bunge unaojadili
Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Kiuchumi kwa mwaka 2014/2015, Mheshimiwa Mbowe
alitahadharisha kuwa hatua ya kujitoa EAC itakuwa na athari mbaya kwa wananchi.
Aidha, siku ya Jumanne, Mh. Mbowe aliwatahadharisha
baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakitoa kile alichokiita kuwa ni maneno
makali dhidi ya mataifa mengine wanachama wa EAC.
Mapema Jumatano, baadhi ya Wabunge waliishinikiza
serikali ijitoe EAC au ifanye mpango wa kuunda jumuiya nyingine kwa
kuzishirikisha nchi nyingine au Tanzania iache kujihusisha na shughuli za
kikanda.
Wabunge walielezea wasiwasi wao juu ya ‘muungano wa
hiari’ ulioundwa na Kenya, Uganda na Rwanda, ambao walisema kuwa wanajihusisha
na shughuli na mazungumzo mbalimbali bila kuzihusisha nchi za Tanzania na
Burundi.
Kwa mujibu wa Wabunge hao, mataifa hayo matatu yamekuwa
yakizungumzia itifaki na mpango wa kuharakisha uundwaji wa shirikisho la
kisiasa.
Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela alisema
kuwa itakuwa bora kama Tanzania itaacha kujihusisha kabisa na masuala
yanayoihusu Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naye mbunge wa viti maalumu (CUF) Bi Rukia Ahmed,
aliitaka serikali kupeleka muswada bungeni wa kutaka kujiondoa katika Jumuiya
hiyo.
“Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mheshimiwa Bernard Membe, alinukuliwa akisema kuwa nchi yetu inachokisubiri ni
talaka tu kutoka kwa washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa nini tukae
na kusubiri talaka, kwa nini tusichukue hatua na kuipata Talaka EAC?” alihoji.
Hata hivyo, Mheshimiwa Mbowe alikosoa mtazamo wa wabunge
wenzake akionya kuwa hatua ya Tanzania kujitoa itakuwa na athari hasi kwa
wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki.
“Ninawaomba wanasiasa wenzangu kujizuia kutoa maneno
yanayoweza kuyaumiza mataifa mengine; wajizuie kutoa matamko yanayoweza kuleta
wasiwasi wa kidiplomasia kati yetu (Tanzania) na nchi nyingine,” alisema
Mheshimiwa Mbowe.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Mbowe, Tanzania na wanachama
wengine wa EAC wanatakiwa kujikita katika mazungumzo ya kidiplomasia ili
kutafuta sulushisho la mkwamo wa sasa unaoikabili Jumuiya hiyo.
“Sisi (Tanzania) tumekuwa tukisifiwa kama miongoni mwa
nchi zenye uwezo mkubwa sana wa kidplomasia duniani, sasa ninashangaa
kinachotutokea sasa,” alisema kiongozi huyo wa kambi rasmi ya Upinzani.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge, Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alibainisha kuwa haikuwa sahihi
kwamba Tanzania itaondolewa katika Jumuiya hiyo.
Waziri Sitta pia alieleza kuwa Tanzania ambayo imekuwa
ikitengwa na washirika wake wa Jumuiya hiyo, inafanya mpango wa kuwa na
uhusiano madhubuti wa kiuchumi na kibiashara na nchi za Burundi na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
CHANZO: THE CITIZEN
0 comments:
Post a Comment