
WATU wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kuwa wanachama wa kundi la
Al-Shabaab. Washitakiwa hao waliofikishwa mahakamani jana ni Ally Rashid,
Shaban Waziri, Faraji Ramadhani na Mussa Mtweve.
Wakili wa Serikali, Peter Maugo alidai mbele ya Hakimu
Mkazi Sundi Fimbo kuwa, kati ya Januari 11 mwaka jana na Septemba 16 mwaka huu,
eneo la Kibaoni Dar es Salaam, Rashid alisajili washitakiwa wenzake kuwa
wanachama wa kundi hilo.
Aliendelea kudai kuwa, katika siku hizo, washitakiwa
walikamatwa kwa kuwa wanachama wa kundi la Al Shabaab ndani ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, ambalo pia linafanya shughuli zake Kenya na Somalia.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu mashitaka kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu ya
Tanzania.
Aidha, upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi
hiyo bado haujakamilika na washitakiwa walirudishwa rumande hadi Desemba 5 kesi
hiyo itakapotajwa.
Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama ya Kisutu katika
hatua ya upelelezi na baadaye itahamishiwa Mahakama Kuu kusikilizwa.
WANAVYOSAJILIWA
Septemba mwaka huu, Shirika la Habari la Uingereza
(BBC), lilitoa taarifa fupi ya namna vijana walivyokuwa wakisajiliwa kujiunga
na kundi hilo katika pwani ya Kenya.
Taarifa hiyo ilitoka baada ya Al Shabaab kukiri kufanya
shambulizi katika jengo lenye maduka makubwa la Westgate jijini Nairobi, ambapo
watu wapatao 60 waliuawa na mamia kujeruhiwa.
Uchunguzi wa BBC ulibaini kuwa vijana hao kabla ya
kusajiliwa walikuwa wakipitia mafunzo yanayopotosha itikadi za dini katika
kuwaandaa kujiunga na kundi la Al shabaab.
Vikao vya kusajili vijana hao ilidaiwa huanza na
viongozi wa dini walio tayari kutoa mafunzo hayo, ili watoe hotuba za namna
hiyo kwa vijana.
Uchunguzi huo umebaini kuwa vijana hao, hufundishwa
kujitolea kupigania kwa kile wanachosema ni dini, na baadaye hupelekwa vijijini
katika maeneo yanayopakana na fukwe za bahari kujiandaa na safari kwenda
Somalia.
CHANZO: HabariLeo
0 comments:
Post a Comment