
Siku moja baada ya wabunge kuwataka Waziri Mkuu
Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki kujiuzulu kwa
kushindwa kusimamia Operesheni Tokomeza Ujangili, pembe 706 za ndovu
zimekamatwa jijini Dar es Salaam.
Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa katika
hifadhi za wanyama pori mbalimbali hapa nchini. Tukio hilo lililotokea jana
jioni katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni, wilayani Kinondoni, liliongozwa na
Waziri Kagasheki ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Tarish Maimuna.
Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe za ndovu ni
raia watatu wa China ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka
mji wa Guandung .
Raia hao wa China wamekuwa wakiishi katika nyumba
hiyo kwa miaka mingi wakifanya biashara ya kuingiza nchini vitunguu swaumu
kutoka China na kusafirisha nje ya nchi makombe yanayopatikana baharini.
Alipoingia ndani ya nyumba hiyo, Kagasheki ambaye
aliambatana na askari polisi na baadhi ya maofisa usalama alishuhudia shehena
kubwa ya pembe za ndovu ikiwa imehifadhiwa kwenye viroba vyenye uzito wa kilo
50.
Mbali ya kushuhudia shehena ya pembe hizo,
alionyeshwa gari maalumu aina ya Toyota Noah ambalo watuhumiwa hao hulitumia
kutoa pembe porini na kuyaingiza jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika eneo la tukio mara baada ya
kuwakamata alisema kukamatwa kwa watu hao kunatokana na matokeo ya Operesheni
Tokomeza Ujangili ambayo imesitishwa na Serikali juzi baada ya wabunge
kuilalamikia.
Waziri Kagasheki alisema kwamba katika harakati za
kutaka kuwakamata watuhumiwa hao walitoa Sh30 milioni kwa ajili ya kujaribu
kuwahonga askari.
“Walitaka kuwahonga askari ili wasikamatwe,” alisema
huku akionyesha noti za fedha hizo.
Alisema wabunge wanaomtaka ajiuzulu kwa madai kwamba
Operesheni Tokomeza Ujangili imesababisha mauaji ya watu na mifugo wanapoteza
muda kwa kuwa mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete pekee.
“Sasa mimi nasema kunitoa haitakuwa rahisi anayeweza
kunitoa ni yule aliyeniweka,” alisema.
Alisema ipo mikakati inayofanywa na baadhi ya
wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
“Itakuwa ni jambo la ajabu kwamba kila mtu akiingia
madarakani wanataka atoke, watatolewa wangapi?” alihoji na kuongeza kuwa
operesheni hiyo ni muhimu kwa ajili ya kunusuru tembo wasiishe.
Alisema kwamba ni kweli kuna baadhi ya dosari
zimejitokeza kwenye operesheni ikiwamo kuuawa kwa baadhi ya mifugo, lakini siyo
kwamba zoezi zima halina manufaa.
Kagasheki alisema kama kasi hii ya kuuawa kwa tembo
itaachiwa iendelee baada ya miaka 10 tembo wote watakuwa wameisha nchini.
Alisema hataki kuona utawala wa Rais Kikwete ukiondoka
madarakani ukiwa na lawama ya kuachia majangili wawamalize tembo.
Mmoja wa watuhumiwa hao, Huang Qin alisema shehena yote
ya pembe za ndovu iliyokamatwa nyumbani kwake ilikuwa ikiletwa kidogo kidogo na
rafiki yake ambaye hakumtaja jina.
Akiongea kwa Kiswahili Qin alisema: “Mimi hii si yangu,
kichwa yangu mbovu. Rafiki yangu alileta hii (pembe) kidogo kidogo.”
Januari mwaka huu, Gazeti La Daily Mail la Uingereza
liliripoti kwamba Serikali ya Kenya imekamata shehena ya vipande 638 vya pembe
za ndovu ambavyo ni sawa tembo 320 waliouawa.
Mzigo huo wa tani mbili ulikuwa kwenye kontena la mawe
ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa tani nne za pembe za
ndovu zenye thamani ya Dola za Marekani 3.4 milioni sawa na takriban Sh5.4
bilioni zilikamatwa Hong Kong Oktoba 20, mwaka jana, huku ikielezwa kuwa meno
hayo yalikamatwa yakisafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu
Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na pembe
za ndovu yenye thamani ya Sh18.4 milioni yaliyotengenezwa kama bangili tayari
kusafirisha kwenda nje ya nchi.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment