![]() |
| Mbunge wa Wawi,Hamad Rashid Mohammed |
Hali hiyo imejitokeza baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kusema hawajafikiria mwafaka na Hamad kwa kuwa hajaomba msamaha, huku Hamad naye akisema kwa jinsi mambo yalivyo hata kama suluhu itapatikana, bado hakutakuwa na kuaminiana baina yake na chama hicho.
Hamad na wenzake 13, walivuliwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi wa CUF, kwa madai ya kuchochea vurugu katika chama hicho.
Hata hivyo, Hamad na wenzake hawakuridhika na uamuzi huo, na kuamua kufungua kesi ya kupinga katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
Profesa Lipumba alisema tangu Hamad avuliwe uanachama, hajachukua hatua zozote za kuomba msamaha dhidi ya tuhuma zilizosababisha achukuliwe hatua hiyo licha ya muda mrefu kuwa na nafasi ya kufanya hivyo.
Hivyo, alisema haoni pa kuanzia kusema kama wako tayari kufikia mwafaka na Hamad au la.
“Kafulila (David) amezungumza na NCCR-Mageuzi ndiyo wakafikia mwafaka. Alianza Kafulila kuomba msamaha ndiyo NCCR-Mageuzi wakafikia maamuzi hayo (ya kumrejeshea uanachama),” alisema Profesa Lipumba.
Kwa upande wake, Hamad alisema ni vigumu kufikia mwafaka baina yake na CUF kwa sababu mbili kuu.
Sababu ya kwanza ni kauli iliyowahi kutolewa hadharani na baadhi ya viongozi wa CUF siku chache kabla ya kuvuliwa uanachama kwamba, “Ama Hamad aisambaratishe CUF au CUF imsambaratishe Hamad”.
“Kwa bahati nzuri nikaenda mahakamani kuonyesha kwamba, si kila linaloamuliwa na chama lina uhalali,” alisema Hamad.
Alisema pamoja na hatua hiyo, anajivunia pia uamuzi wa kuruhusiwa kwa mgombea binafsi nchini, kwani kabla ya hapo vyama vilikuwa vikitumia mwanya huo kuwakomoa wanachama wake.
Hamad alisema suluhu ya kweli baina yake na CUF kamwe haiwezi kufikiwa kwa sababu kuna mambo ndani ya chama hicho, ambayo hakubaliani nayo.
Alisema hadi sasa msimamo wa viongozi wa CUF Tanzania Bara na Zanzibar katika baadhi ya mambo, kama vile idadi ya serikali zinazotakiwa kuundwa, unatofautiana.
Hamad alisema pia katika CUF kuna tatizo, ambalo bado halijarekebishwa. Alilitaja tatizo hilo kuwa ni chama kutofanya kazi kama taasisi na taratibu za kushughulikia migogoro kutoheshimiwa.
“Ndiyo maana kina (aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum-CUF, Naila) Jidawi (na wenzake) walipofukuzwa katika chama walikwenda mahakamani,” alisema Hamad na kuongeza: “Bahati mbaya mpaka sasa chama hakiendi kwenye mstari. Ni vizuri turudi kwenye mstari.”
NCCR-Mageuzi wiki iliyopita kilitangaza kumaliza tofauti kati yake na Kafulila, kwa kukubaliana kumrudishia uanachama wake na kufuta kesi ya kupinga kuvuliwa uanachama iliyofunguliwa na mbunge huyo aliyevuliwa uanachama Desemba 17, 2011 kwa madai ya kuchochea vurugu.
Hata hivyo, Kafulila alifungua kesi ya kupinga katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment