SHEIKH PONDA ATOROSHWA MUHIMBILI





*Polisi waingia wodini wakiwa na mavazi ya kidaktari

*Familia yake yaduwaa, Waislamu kutoa tamko leo 

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ametoroshwa wodini na watu wanaodaiwa kuwa ni polisi, huku familia yake ikipigwa na butwaa.

Ponda aliondolewa jana saa 4: 30 asubuhi, katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (MOI), mahala alipokuwa akitibiwa jeraha linalodaiwa kuwa lilitokana na kupigwa risasi mkoani Morogoro.

Sheikh Ponda ambaye juzi alisomewa mashtaka ya uchochezi akiwa kitandani, alichukuliwa na watu hao ambapo mmoja wao alionekana akiwa amevalia koti la kidaktari na wengine wakiwa wamevaa sare za Jeshi la Polisi. Baada ya kutolewa wodini, Ponda aliingizwa katika gari moja Land Cruiser Hard Top yenye namba za usajili T 140 BLA, akiwa chini ya ulinzi mkali.

Miongoni mwa watu waliomchukua Sheikh Ponda pia yumo kachero mmoja kutoka kituo kikuu cha Polisi cha jijini Dar es Salaam, ambaye alitambuliwa kwa jina moja la Hassan.

Akizungumza na MTANZANIA jana, msemaji wa familia ya kiongozi huyo wa dini, Is-haka Rashidi alisema kama familia wameshangazwa na kitendo hicho huku wakiwatilia shaka watu waliomchukua.

Rashidi alisema, Sheikh Ponda hakustahili kufanyiwa kitendo hicho kwa kuwa alikuwa bado akiendelea na matibabu na kwamba afya yake bado haijaimarika.

“Leo aliingia daktari mmoja ambaye toka Ponda amelazwa hakuwahi kumtibu hata siku moja, alimuambia kuwa amepata karatasi ya discharge (ruhusa) na kutakiwa kuondoka hospitali.

“Mara daktari huyo ambaye hakujitambulisha jina wala kuonesha kitambulisho alipotoka nje, waliingia askari polisi na kumwambia Ponda anatakiwa kuondoka kutokana na maagizo ya daktari na hatimaye waliondoka naye,” alisema Rashid.

Rashid aliongeza kusema: “Baadhi ya ndugu pamoja na mke wa Ponda waliokuwepo hospitalini, waliwahoji wanampeleka wapi, walijibiwa na polisi kuwa wasiwe na wasiwasi kwani Ponda yupo katika mikono salama.

“Kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda ni kitendo kibaya hakina tofauti na utekaji, hakutendewa haki kama mgonjwa, wamemchukua kwa hila na dawa zake hawakuchukua wakati wanajua Ponda ni mgonjwa, hii kweli ni haki?” Alihoji.

Rashid alisema hadi saa 6 mchana jana familia ilikuwa haina taarifa kuhusu mahala alipopelekwa Sheikh Ponda, lakini baadaye walipata taarifa kuwa amepelekwa katika gereza la Segerea.

Rashid alisema wao kama familia hawana la kufanya isipokuwa suala la Sheikh Ponda wamelikabidhi katika taasisi yake (Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania), kwamba wao watajua cha kufanya.

Alisema walipokwenda kuomba hati ya Ponda kupewa ruhusa, ndipo walipoambiwa kuwa ndugu yao alikuwa amechukuliwa na polisi na kwamba ruhusu hiyo ilikuwa imetolewa na Dk. mmoja aliyemtaja kwa jina la Swai.

“Tulipouliza kuhusu gharama za matibabu, madaktari walituambia gharama ni Sh 1,100, 000 na kutuambia tukitaka tuilipe au tusiilipe. Sasa hatujui kama Serikali italipa au ni MOI yenyewe,” alisema.

WAKILI WA PONDA

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, Wakili wa Ponda, Juma Nassoro alisema Sheikh Ponda amepelekwa Segerea na askari Polisi.

“Kuchukuliwa kwake sisi hatukuridhika kutokana na kuwa sijafahamishwa na hali yake sio nzuri, kutokana na kitendo hicho tutachukua hatua tukikamilisha tutawafahamisha.

POLISI YAZUIA MAANDAMANO

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limezuia maandamano yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo kwa ajili ya kupinga na kulaani kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda cha kupigwa risasi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso alisema maandamano hayo hayawezi kuruhusiwa kwa kuwa uchunguzi juu ya suala hilo unafanywa.

“Jeshi la Polisi linawaonya wananchi wote watakaofanya vurugu, fujo au maandamano yasiyo na tija kwa lengo la kuvunja amani kwamba watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Senso.

Senso alisema Jeshi la Polisi lilikwishaunda tume maalumu kwa ajili ya kuchunguza suala hilo lililotokea Agosti 10, mwaka huu mkoani Morogoro wakati Ponda akihutubia mkutano wa kidini.

Alisema kwa mujibu wa sheria, askari yeyote atakayefyatua risasi hewani iwe ni kwa kujihami au kutawanya fujo kwa bahati mbaya, lazima lifunguliwe jalada la uchunguzi.

Senso alisema Jeshi la Polisi linamshikilia askari aliyefyatua risasi hewani mkoani Morogoro, kwa ajili ya mahojiano pamoja na kufanya uchunguzi wa tukio hilo.


CHANZO: Mtanzania
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment