YANGA YAPINGA UDHAMINI WA AZAM

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga




Uongozi wa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Yanga jana  ulitangaza nia yake ya kukataa mechi zao za ligi hiyo kuonyeshwa moja kwa moja kupitia kituo cha televisheni kinachomilikiwa na kampuni ya Azam Media ambayo ndiyo inaimiliki klabu mojawapo hasimu katika ligi hiyo ya Azam FC.

Mwishoni mwa wiki, Shirikisho la Soka Tanzania kupitia Bodi yake ya Ligi Kuu (TPL) liliingia mkataba wa miaka mitatu na Azam wenye thamani ya Sh. bilioni tano.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema kuwa Kamati ya Utendaji ya timu yake iliyokutana juzi ndiyo iliyoamua kupinga udhamini huo kwa nia ya kulinda maslahi ya klabu yao na wamefanya hivyo kwa sababu wanatambua thamani yao.

Sanga alisema kwamba kiasi cha fedha kilichoamuliwa kulipwa kwa klabu ni ndogo na maamuzi hayo hayaingilii maamuzi yaliyofanywa na timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo inayotarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 24 mwaka huu.

"Sisi (Yanga) tuna thamani tofauti na klabu nyingine.

Haiwezekani klabu yenye wanachama wengi na wapenzi wengi tupate kiasi sawa na klabu ndogo au zinazomilikiwa na taasisi," alisema Sanga.

Aliongeza kwamba baada ya kutoa maamuzi hayo, pia wana mpango wa kukutana na wanachama wao ili kupokea mawazo yao na hatimaye kueleza msimamo wao wa mwisho.

Alisema pia utaratibu wa kuipa Azam Media haki ya kuonyesha mechi zote za Ligi ya Bara ulikiukwa kwa kutotangazwa kwa tenda kama inavyofanyika katika mashindano mengine na vilevile, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi Kuu, Said Mohammed, alipaswa kujiuzulu na asishiriki katika maamuzi ya kuipa haki kampuni anayofanyia kazi ili kuepuka mgongano wa maslahi.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo iliyopewa haki ya kuonyesha mechi za ligi inaangalia maslahi yake binafsi ambapo kama kuna matangazo ya pombe, kamwe haitaonyesha wakati wao wanadhaminiwa na bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Vile vile alisema kwamba kiasi cha Sh. milioni nane kwa mwezi kwao ni kidogo mno kwani hivi sasa, mapato yao wanayopata ni zaidi ya Sh. milioni 50 na mechi zikirushwa hewani zitapunguza mashabiki wanaofika uwanjani.

"Tuna wasiwasi kwamba imekuja kwa nia ya kutumaliza sisi kwa sababu tuna kikosi chenye nguvu na wao pamoja na wapinzani wetu wameamua kujihami," alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Abdallah Binkleb.

Aliongeza kuwa pia wanahofu huenda wachezaji wa Yanga watakapofanya rafu za kimchezo picha zao kurudiwa mara kwa mara na pale mchezaji wa Azam atakapofunga goli huku akiwa ameotoa kutorudiwa kwa picha hiyo.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa tayari makubaliano hayo yamefanyika na shirikisho hilo lilifanya mazungumzo na makampuni mbalimbali kabla ya kufikia maamuzi ya kuingia mkataba na Azam Media.

Wambura alisema kuwa endapo Yanga itaendelea kuwa na msimamo huo, basi kitakachofanyika ni kutoonyeshwa kwa mechi zake za nyumbani lakini za ugenini zitarushwa hewani.

Katika mkutano mkuu wa klabu ya Simba uliofanyika Julai 20 mwaka huu, mwenyekiti, Aden Rage, alitangaza kwamba klabu hiyo inapendekeza udhamini wowote utakaopatikana katika ligi ugawiwe sawa kwa timu zote.

Kauli hiyo ya Rage ilikuja siku mbili baada ya Simba kusaini mkataba na Azam Media ili kuonyesha kipindi chake cha televisheni kiitwacho Simba TV Show.


CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment