WATU ZAIDI WAUAWA NCHINI MISRI






Kitengo cha huduma za dharura nchini Misri kimeripoti kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha katika shambulizi la jeshi dhidi ya waandamanaji wanamuunga mkono rais aliyeendolewa madarakani, Muhammad Mursi, imefikia watu 51.

Wizara ya afya pamoja na kitengo cha huduma za dharura zimesema leo kuwa zaidi ya watu 50 waliuawa wakati wa makabiliano baina ya jeshi na wafuasi wa Mursi nje ya makao makuu ya Walinzi wa Jamhuri.

idadi hiyo iliongezeka kufikia 51 baada ya majeruhi waliokuwa hospitali kufariki dunia.

Duru kutoka hospitalini zinasema kuwa vifo vinatarajiwa kuongezeka kwa sababu baada ya majeruhi wapo katika hali mbaya.

Hali hiyo imekuja baada ya jeshi kuwafyatulia risasi wafuasi wa chama cha Udugu wa Kiislamu - Muslim Brotherhood – mjini Cairo, hatua iliyokifanya chama hicho kutangaza maasi dhidi ya jeshi.


Jeshi linasema kuwa liliwakabili watu wenye silaha waliokuwa wakijaribu kuingia katika jengo hilo. Msemaji wa jeshi pia alieleza kuwa mwanajeshi na polisi mmoja walipigwa risasi na kufa katika shambulizi hilo.


Hata hivyo, viongozi wa Muslim Brotherhood na madaktari waliokuwa eneo la tukio wameyakanusha vikali madai hayo na kusema kuwa wanajeshi walijaribu kuuvunja mkusanyiko wa wafuasi wa Mursi ambao walikuwa wakiswali.

Madaktari wamelielezea tukio hilo kama mauaji ya kinyama na kwamba watoto kadhaa ni miongoni mwa waliopoteza maisha.


Wakati huo huo, uongozi wa mpito wa nchi hiyo umeelezea masikitiko makubwa kwa wale waliouawa katika tukio hilo na kusema kuwa wameunda kamati ya kimahakama kufanya uchunguzi.

Nje ya Misri, Uturuki, Umoja wa Ulaya, Qatar na harakati ya mapambano ya Kipalestina ya Hamas, wamelilaani tukio hilo.

Misri imeshuhudia maandamano ya mahasimu wa kisiasa baina ya wafuasi na wapinzani wa rais aliyeondolewa madarakani na hivyo kutumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa.


Mursi aling’olewa madarakani kwa nguvu Julai 3, na Mkuu wa Mahakama ya Katiba Adly Mansour, akaapishwa kuwa rais wa muda wa Misri tarehe 4 Julai.


Inasemekana kuwa Mursi ameshikiliwa na jeshi. Maafisa waandamizi wa jeshi wanasema kuwa anaweza kufunguliwa mashitaka rasmi kuhusu tuhuma zilizotolewa na wapinzani wake.


hati kadhaa zimetolewa kwa ajili ya kukamatwa kwa wanachama wa Muslim Brotherhood. Hivi karibuni askari na vikosi vya usalama wameongoza harakati zao za kuwatia nguvuni viongozi wakubwa wa kisiasa wa Muslim Brotherhood waliokuwa na ukaribu na Mursi.


Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment