MISRI IKO NJIA PANDA
Mkuu wa jeshi la Misri, Jenerali Abdulfattah al-Sisi ameitisha maandamano ya nchi nzima siku ya Ijumaa kumpa mamlaka ya kupambana na kile alichokiita kuwa ni vurugu na ugaidi kufuatia kuondolewa madaraka kwa Rais Muhammad Mursi.
"Ijumaa ijayo, waheshimiwa wananchi wote wa Misri waingie mitaani kunipa nguvu na mamlaka ya kukomesha ugaidi na ghasia," alisema katika hotuba aliyoitoa leo wakati wa sherehe za kumaliza mafunzo ya kijeshi.
Jenerali Sisi alikanusha tuhuma za kumsaliti Mursi na kuapa kushikamana na mpango wa ramani ya amani iliyowekwa ili kufanya mabadiliko ya katiba na kufanyika kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika ndani ya miezi sita.
Al-Sisi, mbali na cheo chake cha ukuu wa majeshi, ni Naibu Waziri mkuu na Waziri wa Ulinzi katika serikali ya mpito ya nchi hiyo.
0 comments:
Post a Comment