| Waokoaji wakimbeba majeruhi baada ya mlipuko uliotokea kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu leo Juni 19, 2013. |
Kwa uchache watu 15 wamepoteza maisha katika shambulio lililofanywa kwenye ofisi kuu ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Maafisa usalama wa ndani wanasema kuwa mlipuaji alitupa vitu vyenye mlipuko kwenye ofisi ya Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) leo jumatano.
Baada ya mlipuko huo, watu kadhaa wenye silaha nzito waliingia katika eneo hilo la kufanya mashambulizi.
Hata hivyo, polisi wanasema kuwa hali ya mambo imedhibitiwa na vikosi vya serikali vinafanya ulinzi kwenye jengo hilo.
Majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya jirani, lakini idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka kwa sababu baadhi ya majeruhi wanasemekana kuwa katika hali mbaya.
Mara nyingi wapiganaji wa al-Shabab wamekuwa wakidai kuhusika na mashambulizi kama hayo. Mji mkuu wa Somali umekuwa ukishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara tangu wapiganaji hao walipoondolewa katika mji huo miaka miwili iliyopita.
Somalia imekuwa na serikali dhaifu tangu mwaka 1991, baada ya wababe wa kivita kumuondosha madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Siad Barre.
Hata hivyo, kikao cha wabunge kilichofanyika Septemba 2012 mjini Mogadishu kilimchagua Hassan Sheikh Mohamud kwa kura nyingi kuwa rais mpya wa Somalia.
0 comments:
Post a Comment