TBL YAZUA MTAFARUKU KKKT


MTAFARUKU mkubwa umeibuka ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) baada ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuchangia harambee ya Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kanisa hilo cha Tumaini. Hatua hiyo imesababisha aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa hilo, Mkumbo Mitula wa Usharika wa Hananasifu, kujiuzulu akipinga kanisa kuruhusu kampuni ya pombe kuchangia fedha wakati haliruhusu ulevi.


Pia katika kikao cha kila mwezi cha viongozi wa kanisa hilo kilichofanyika Usharika wa Magomeni hivi karibuni, Mchungaji Mitula, aliwaeleza viongozi hao kuwa ni vyema wakatubu kwa kitendo cha kuruhusu Kampuni ya Bia kuchangia harambee kanisani, kwani wamelinajisi kanisa.


Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Mchungaji huyo aliyejiuzulu zinaeleza kuwa TBL walichangia ujenzi wa chuo hicho mwaka 2011, hatua iliyosababisha achukue maamuzi magumu ya kuachia ngazi.


Hata hivyo baada ya hatua yake hiyo inaelezwa kuwa viongozi wa juu wa kanisa hilo, wamekuwa wakimfuata fuata wakimshutumu juu ya kauli zake ambazo amekuwa akizitoa mbele ya hadhara ya watu akipinga kanisa kunajisiwa na michango ya kampuni inayozalisha pombe.


Pamoja na hilo, semina tatu alizotakiwa azifanye Mchungaji Mitula katika makanisa hayo kuanzia Juni 23 hadi 28 mwaka huu mkoani Mwanza, imeahirishwa ghafla na Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Mwanza, Andrea Gulle.


Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Mchungaji Mitula, alisema kuwa ameshangazwa kwa kitendo hicho cha Askofu Gulle kusitisha ghafla semina hizo.


Alisema hata pale alipojaribu kumuuliza askofu huyo sababu za kusitisha semina hizo, alijibiwa kwamba amewasiliana na wakuu wake wapatane ndipo ataruhusu semina ziendelee.


Alisema aliamua kujitoa katika utawala wa kanisa hilo, kutokana na mambo hayo ya kuruhusu kampuni ya pombe kuchangia harambee, jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya kanisa na hata imani ya kiroho hairuhusu pombe kanisani.


“Kuna uvumi mwingi umesikika kuwa mimi nimefukuzwa na kanisa, ninawaomba wote niliowahi kuwahudumia kiroho wafahamu kuwa, nilijiuzulu mwenyewe kutokana na mambo hayo ya ajabu kuruhusiwa kanisani, huku Askofu Mkuu, Alex Malasusa akifurahia hayo,” alisema Mitula.


Pia alisema kitu kingine ambacho kimemfanya ajitoe katika kanisa hilo, ni kutokana na karani ambaye alikuwa akifanya matumizi ya fedha bila idhini yake na hata pale alipomuonya alikaidi.


“Pale nilipomchukulia hatua kwa kumsimamisha kazi, uongozi wa kanisa ulinikomoa kwa kumrudisha kwa nguvu na kunidhalilisha kwa kuniandikia tuhuma za kuvunja taratibu za ajira za DMP,” alisema.


Alisema baada ya mlolongo wote huo, hakuona haja ya kuendelea kutumikia ufalme uliofitinika, hivyo akajiwajibisha mwenyewe kwa kujitoa.



MTANZANIA Jumapili lilimtafuta Askofu wa kanisa hilo, Alex Malasusa kupitia simu yake ya kinganjani, ili aweze kuthibitisha madai ya mchungaji huyo, lakini baada ya kusikiliza maelezo ambayo yalitakiwa yapatiwe ufafanuzi akauliza; “unamfahamu Negida” gazeti hili liliposema halimfahamu akasema “ngoja nikutumie mawasiliano yake” jambo ambalo hakufanya.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment