*Kamati Kuu yakutana kujadili rasimu ya Katiba
*Hoja ya Serikali tatu kutawala mjadala
*Dk. Chegeni, Lipumba watoa msimamo mkali
*Hoja ya Serikali tatu kutawala mjadala
*Dk. Chegeni, Lipumba watoa msimamo mkali
KIVUMBI cha majadiliano ya Rasimu ya Katiba mpya, kinatarajia kutimka leo, wakati Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), itakapokutana mjini Dar es Salaam kupitia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba wiki iliyopita.
Habari za kuaminika zilizopatikana mjini Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na uongozi wa juu wa CCM, zinasema kikao hicho kitaongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
“Ndugu kesho (leo), CC inakutana chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete na moja ya mada kubwa ambayo inaweza kutawala kikao hiki, ni pendekezo la kuunda Serikali tatu kama ilivyotolewa na Jaji Joseph Warioba (Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba).
“Kama unavyojua, tangu kutangazwa kwa rasimu hii, watu wamekuwa wakitoa mawazo mbalimbali juu ya muundo huu, nategemea hata CCM kesho (leo), inaweza kuja na jambo jipya, naomba waandishi mjaribu kuwa na subira, tukimaliza kikao kama kawaida tutawaita,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho, kinasema tangu mapendekezo hayo yatolewe, CCM imepokea kwa hisia tofauti, ikitambua wazi mfumo wa uendeshaji wa Serikali ni gharama kubwa kwa wananchi.
Chanzo hicho, kiliiambia MTANZANIA kama mfumo huo utajadiliwa na hatimaye wananchi kuukubali, ni wazi CCM itakuwa na hofu kubwa ya kupoteza nguvu za mamlaka ya dola, tofauti na ilivyo sasa.
Katika rasimu ya Jaji Warioba, alipendekeza muundo wa Serikali ya Zanzibar, Tanzania Bara na Jamhuri ya Muungano.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana alipoulizwa na waandishi wa habari, alisema hapendi kuzungumzia suala hilo kwa kina hadi leo CC itakapokutana.
Lakini wachunguzi wa mambo, walio ndani ya CCM, wanaeleza iwapo muundo wa Serikali tatu za Zanzibar, Tanzania Bara na ile ya Jamhuri ya Muungano kama zilivyopendekezwa na Tume ya mabadiliko ya Katiba utaridhiwa, CCM kinaweza kuambulia ukuu wa Serikali ya Muungano pekee.
Imani hii ya wadadisi na wafuatiliaji wa mambo, inajengwa katika msingi wa uungwaji mkono na wananchi kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa upande wa Tanzania Bara na Chama cha Wananchi (CUF), kwa upande wa Zanzibar.
Kwa msingi huo, haina shaka kuwa CUF ambacho kina nguvu kubwa ya kisiasa kwa upande wa Zanzibar, kinaweza kuibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha urais, huku Chadema kinachoendelea kujipatia umaarufu na uungwaji mkono mkubwa wa wananchi, kikichukua udhibiti wa Serikali ya Tanzania Bara na kukiacha CCM kikibaki na udhibiti wa Serikali ya Muungano, ambayo kinaweza kushinda kutokana na historia yake ya kusaka ushindi wa jumla.
CUF
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema kuna hatari ya Watanzania wakapata Katiba ya nchi ambayo haitokani na maoni yao kwa mujibu wa sheria.
Kutokana na hali hiyo, Profesa Lipumba amemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba kutoharakisha mchakato huo, hadi pale itakapopatikana rasimu ya Katiba kwa upande wa Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba, alisema katika uchambuzi wa awali uliofanywa na CUF, umebaini upungufu kadhaa katika rasimu hiyo.
Alisema katika mapendekezo yake ya msingi, ni kwamba kura ya maoni isubiri kukamilishwa kwa rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara na pindi zikijadiliwa, zijadiliwe kwa pamoja na wananchi.
“Wananchi wamechoka, wanataka mabadiliko na katika hili ni lazima iandaliwe pia na rasimu ya Katiba kwa upande wa nchi ya Tanzania Bara, ili ziweze kujadiliwa zote kwa pamoja na kupigiwa kura ya maoni na Watanzania wote,” alisema Profesa Lipumba.
Akizungumzia ibara ya 181 (4), ya rasimu hiyo ya Katiba, Profesa Lipumba alipinga hatua ya kupendekeza watu wanaotakiwa kuomba kazi hiyo, lazima wawe majaji wa Mahakama Kuu.
“Jambo hili, halikubaliki hata kidogo, eti wanaotakiwa kuomba kazi ya uenyekiti ni lazima wawe majaji wa Mahakama Kuu, kwani kazi hii ni vema iwe inaombwa na mtu yeyote mwenye sifa na tukiondoe kigezo hiki.
Bunge
Alisema katika rasimu hiyo, imeshindwa kufafanua namna ya upatikanaji wa majimbo zaidi ya kutoa tafsiri ya jumla ya kuwa kila mkoa utakuwa na jimbo la uchaguzi na wilaya kwa upande wa Zanzibar, ambapo kila mkoa utakuwa na wawakilishi wawili.
“Hapa tunahitaji namna ya majimbo haya yatakavyopatikana na sio kufanya ujumla kama ilivyo katika rasimu hii ya sasa iliyotolewa na Jaji Warioba,” alisema.
Urais
Profesa Lipumba, alipinga sifa ya kuwa na mgombea urais mwenye shahada ya kwanza, huku akionya kuwa kuna hatari ya nchi kuingia katika uchakachuaji wa vyeti hasa kwa wagombea wengi wa nafasi hiyo.
DK. CHEGENI
Kwa upande wake, Mbunge wa zamani wa Busega Dk. Raphael Chegeni (CCM), amepinga mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba juu ya Katiba mpya na kusema kuwa mfumo wa marais watatu haufai kwa taifa.
Alisema hatua ya kuwa na marais watatu, inaweza kula njama ya kumhujumu Rais wa Muungano.
Akizungumza na MTANZANIA jijini hapa jana, Dk. Chegeni alisema mapendekezo hayo, hayapaswi kuungwa mkono kwani hauwanufaishi Watanzania na kuwa ni kuongeza gharama za uendeshaji na kuchezewa fedha za Watanzania.
“Ikianza kutokea misuguano ya namna hii juu ya nani mwenye madaraka kamili, ni rahisi kwa marais wa Zanzibar na Bara kuamua kula njama ya kumuondoa Rais wa Jamhuri ya Muungano, kutokana na kuingilia uendeshaji wa Serikali mojawapo. Hapo ndipo zinapoweza kuanza njama za kumuhujumu ili aondoke madarakani,” alisema Dk. Chegeni.
CHANZO: Mtanzania

0 comments:
Post a Comment