SITTA ATANGAZA TIMU YAKE


Katika kile kinachoonekana ni mbio za urais 2015, makada wanne wa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameunganisha nguvu tayari kwa kinyang’anyiro hicho.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ni kama ametangaza timu yake ingawa si rasmi pale alipoweka hadharani majina ya makada hao akisema kuwa ni marafiki zake wa karibu ambao wana mikono misafi.
Sitta ambaye anatajwa kuwa  mmoja wa makada watakaowania urais 2015, aliwataja marafiki zake hao juzi wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki la Josephen Bakita, Parokia ya Igoma Mwanza.
Waliotajwa kuwa ni marafaki wa Sitta ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe.
“Membe, Magufuli na Mwakyembe ni marafiki zangu wa karibu ambao wana mikono safi na wameniunga mkono siyo wengine walafi, waongo wanaotutumbukiza katika mikono ya Dowans na Richmond ambao siyo waadilifu na wazalendo;
“Tuwakatae maana ukiwapa madaraka wataweka vibaraka wao na nchi itaelekea pabaya na hiyo ndiyo inaweza kuzusha vurugu kwani ukimnyonya maskini na akiona unamnyonya atataka kufurukuta...Huo ndiyo mwanzo wa vurugu, nchi haiwezi kutulia kwa hiyo tuwakatae watu wa namna hiyo,” alisisitiza Sitta.
Hii ni mara ya kwanza kada huyo wa CCM ambaye amewahi kuliongoza Bunge la Jamhuri wa Muungano kuwataja hadharani marafiki zake hao ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa katika duru za kisiasa nchini.
Katika harambee hiyo Sitta aliwasilisha zaidi ya Sh25 milioni ambazo alisema kati ya fedha hizo Sh5 milioni zilitoka kwa Waziri Membe, Sh5 milioni zingine zilichangiwa na Dk Mwakyembe na Dk Magufuli huku yeye (Sitta) akichangia Sh5 milioni  na pesa zilizobaki zilichangwa na wabunge wanaowaunga mkono.
Sitta alitaja viongozi wengine ambao wanashirikiana vizuri na wamemsadia katika harambee  hiyo kuwa ni Anna Kilango, Merry Nagu, William Geleja, Aden Rage, Catherin Majige, James Lembeli, Mark Mwandosya pamoja na Victor Mwambalaswa ambao wao wote walimchangia Sh500,000  kila mmoja huku Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Lazaro Nyalandu akitoa Sh1 milioni.
Awali Sitta aliwataka Watanzania kuthamini kura zao ili wasiangukie katika mikono ya viongozi mafisadi.
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment