Maslahi binafsi bungeni: Madabida azidi kuwekwa kikaangoni

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zarina Madabida


Hali ya kisisasa na uhusiano kwa jamii si shwari kwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zarina Madabida.

Hali hiyo inatokana na kuzidi kubanwa na taasisi ‘alizozizushia’ bungeni, ambazo hata hivyo, kwa nyakati tofauti zimemkosoa Mbunge huyo.

Baada ya uongozi wa NIPASHE, kupitia safu ya tahariri ya jana, kukanusha tuhuma za Madabiba, zikiwamo za uongo na kutumika kisiasa, asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Sikika, ‘imemshukia’ na kumtaka aombe radhi.

Sikika, inakanusha vikali tuhuma nyingine iliyotolewa na Madabida bungeni, kwamba inahusika kuandaa maandamano ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi (Waviu).
Kwa mujibu wa Madabida, akizungumza bungeni, maandamano hayo yalipangwa kufanywa dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Mkurugenzi Mtendaji wa Sikika, Irenei Kiria, katika taarifa yake aliyoitoa jana jijini Dar es Salaam, alisema asasi hiyo haijaandaa, wala kufikiria kuandaa maandamano hayo dhidi ya CCM.

Kiria, alisema kinachoonekana kwa Madabida, ni kutafuta huruma ya kutetewa na chama chake kwa makosa yanayoonekana kufanywa na mtu binafsi.

Katika kikao cha Bunge cha Mei 8 mwaka huu, Madabida, akichangia bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliitaja Sikika kwamba imekuwa ikiwakusanya Waviu,na kuwachochea waandamane kwenda ofisi za CCM.

Kiria, alisema wamesikitishwa na kitendo cha Bunge kuruhusu baadhi ya wabunge kutumia muda wa vikao vyake kutetea maslahi binafsi badala ya umma.

Madabida ni mbunge anayetajwa kuwa na maslahi mapana katika umiliki wa kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI), ambacho hivi karibuni kimetuhumiwa kuzalisha ARVs bandia na kuiuzia bohari ya dawa nchini (MSD).

Alisema, kauli ya Madabida, inalenga kuchonganisha na kuharibu muonekano wa Sikika kwa Watanzania wanaofaidika na shughuli au tafiti mbalimbali inazozifanya.
Kiria, alisema haiingii akilini kwa wananchi kuandamana kwenda ofisi za CCM kwa kadhia ya ARVs bandia, kwa sababu wahusika wa suala hilo ni wizara ya afya na polisi.

Sikika ni shirika lisilo la kiserikali lililosajiliwa nchini Tanzania kwa lengo la kufanya utetezi juu ya utawala na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa zenye ubora na viwango.

Kiria, alisema Sikika itaendelea kutetea kwa kadri iwezavyo, bila upendeleo wala uonevu na kuhakikisha Watanzania, wakiwamo wanaoishi na virusi vya ukimwi, wanapata huduma bora za afya, ikiwamo dawa na vifaa tiba.

Hivyo, alisema "tutafuatilia sakata hili hadi ukweli uwekwe wazi na wahusika wachukuliwe hatua. Hata kama itagundulika kuwa wahusika hao ni wabunge, makada wa vyama au watendaji wa serikali."

Wakati akichangia Wizara hiyo, Madabida alisema anazo taarifa kwa Sikika inakusanya Waviu katika mikoa mbalimbali na kuwapeleka ofisi za CCM jijini Dar es Salaam kwa maandamano.
 
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About mahamoud

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 comments:

Post a Comment