*Afutiwa mashitaka ya ugaidi
*Abakiwa na shitaka moja
*Abakiwa na shitaka moja
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imefuta mashtaka yote matatu ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.
Uamuzi huo wa Mahakama ulitolewa jana na Jaji Laurence Kaduri aliyesikiliza maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa Lwakatare kupinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa kumfutia mashtaka mteja wao na kumfungulia upya mashtaka yale yale ya ugaidi.
Upande wa Serikali uliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Ponsian Lukosi na upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Peter Kibatala.
“DPP hakukosea kufuta mashtaka na kuyarudisha tena mashtaka hayo hayo kwa sababu utaratibu ulikosewa, mashtaka ndiyo yanafanya mahakama ianze kufanya kazi, shtaka lazima liwe sahihi, lijieleze na kuwa na taarifa za hali halisi ya makosa anayoshtakiwa nayo muhusika.
“Kwa kesi tuliyo nayo, mashtaka ya ugaidi dhidi ya Lwakatare yalitakiwa kuonyesha huo ugaidi, naunga mkono hoja ya Wakili Tundu Lissu kwamba kulingana na makosa ya ugaidi taarifa zilizopo hazionyeshi uhalisia wa ugaidi.
“Kulikuwa na makosa katika kufungua mashtaka ya ugaidi, kutokana na hali hiyo mahakama inayafuta mashtaka yote kuanzia la pili, tatu na la nne. DPP aendelee na shtaka la kwanza katika mahakama yenye uwezo wa kulisikiliza,”alisema Jaji Kaduri.
Baada ya Jaji Kaduri kutoa uamuzi huo na kutoka mahakamani, Lwakatare alinyoosha mikono akiwa kizimbani na kumkumbatia wakili wake, Kibatala kwa saa kadhaa hadi aliposhtuliwa na askari magereza waliotaka kuondoka naye.
Lwakatare alimkumbatia Kibatala kwa furaha bila kusema kitu na alipomwachia wafuasi wa CHADEMA kila mmoja aliendelea kumkumbatia wakili huyo kwa nyakati tofauti kuanzia ndani ya mahakama hadi nje alipowaaga kurudi kuendelea na kesi nyingine.
Shtaka la kwanza analoendelea kushtakiwa nalo Lwakatare ni la kula njama kinyume cha sheria namba 384 ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2012. Shtaka hilo lina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Inadaiwa kwamba Desemba 28 mwaka jana, Lwakatare na Ludovick wakiwa maeneo ya Kimara Stop Over walikula njama ya kutenda kosa la kumpa kumdhuru Denis Msacky.
Mashtaka yaliyofutwa ni shtaka la kula njama ya kumteka nyara Msacky, shtaka la kufanya mkutano wa kigaidi ambako washtakiwa wote wanadaiwa walishiriki mkutano huo huku wakijua unahusu jinsi ya kumteka Msacky.
Shtaka dhidi ya Lwakatare peke yake kwamba akiwa mwenye nyumba aliruhusu mkutano kati yake na Ludovick ufanyike kwa nia ya kushawishi vitendo vya ugaidi.
Jaji Kaduri alisema makosa hayo yanasikilizwa na Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu awali ilikosea kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa katika jalada namba 37 la mwaka huu na kuwaruhusu washtakiwa kujibu mashtaka.
“Mpaka hapo tunaona kulikuwa na makosa ikiwa ni pamoja na jalada namba 37 kufunguliwa katika kitabu cha usajili wa kesi za mahakama ya chini, DPP alikuwa sahihi kuifuta kesi na kuirudisha tena ambako ilifunguliwa kesi namba 6 ya mwaka huu katika kitabu sahihi cha kesi zinazotarajiwa kuhamia Mahakama Kuu,”alisema.
Awali jopo la mawakili wa Lwakatare waliomba mwenendo wa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu katika jalada 37/2013 na jalada namba 6/2013 upitiwe upya.
Waliomba mahakama itengue hati ya kufuta mashtaka iliyotolewa na DPP, iridhie uamuzi wa dhamana uliotakiwa kutolewa na Hakimu Emilius Mchauru katika kesi namba 37 utolewe, mahakama iliondoe jalada namba 6 linalosikilizwa na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana na itamke kwamba utaratibu wa DPP haukuwa sahihi.
"Tunaomba mahakama ione kuwa kitendo cha DPP kumfutia mashtaka mteja wetu MAchi 18 mwaka huu na kumfunguliwa upya mashtaka yale yale kwa muda mfupi Machi 20 mwaka huu ni kinyume na msingi wa sheria inayomuongoza namna ya kutimiza madaraka,”alidai Kibatala.
Naye wakili Lissu alidai kuwa mahakama hiyo iangalie uhalali wa mashtaka hayo kwa kuwa sheria inasema mkutano kuhusu ugaidi lazima uhusishe watu zaidi ya watatu.
"Kifungu namba 26(2) cha sheria ya ugaidi kinaeleza wazi kuwa mkutano wa ugaidi lazima uhusishe watu zaidi ya watatu na kuendelea tofauti na kesi hii ambako washtakiwa wapo wawili hivyo mashtaka haya hayawezi kusimama," alisema Lissu.
Alidai kuwa mbali na hilo mkutano huo lazima uonyeshe lengo la ugaidi huo lakini katika hati ya mashtaka ya washtakiwa hao haikuonyesha malengo hayo.
Akizungumzia shtaka la kuteka nyara, alidai kuwa shtaka hilo lipo katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu na ya ugaidi na kwamba katika hati ya mashtaka ya washtakiwa hao haikuonyesha shtaka hilo limesimama katika sheria ipi.
Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Prudence Rweyongeza alidai kuwa madaraka ya DPP yamewekwa kisheria na kwamba yametumika vizuri katika kesi hiyo ikiwa ni pamoja na kulinda haki.
"Maombi ya mawakili wa Lwakatare hayana msingi kwani kuruhusu kesi 37/2013 yenye makosa kuendelea kusikilizwa itakuwa kuogelea katika makosa yale yale," alidai Rweyongeza.
Kesi ya Lwakatare na mwenzake inatarajia kutajwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 13 mwaka huu ambako utaratibu mwingine wa sheria utabainika kuhusu shtaka moja linalomkabili ambalo lina dhamana katika sheria.
0 comments:
Post a Comment