Kamanda mkuu wa kundi la al-Nusra Front nchini Syria ameuawa katika mapambano na jeshi la serikali katika mji wa magharibi wa al-Qusayr.
Kwa mujibu wa televisheni ya taifa nchini humo, Kamanda huyo aliyetambuliwa kama Abu Omar aliuawa leo jumanne mjini al-Qusayr wakati mapigano baina ya vikosi vya serikali na waasi hao katika mji wa mpakani yakiingia katika siku yake ya tatu.
Jeshi la Syria linasema kuwa kwa sasa linadhibiti asilimia 70 ya mji huo muhimu, unaunganisha mji mkuu Damascus na bandari ya Tartous katika bahari ya Mediterranea.
Mapambano makali yameripotiwa kuendelea katika baadhi ya maeneo ya mji wa al-Qusayr, karibu kilometa 30 kusini magharibi mwa Homs, huku jeshi la serikali likionekana kusonga mbele zaidi na kuyadhibiti maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi wanaopigana dhidi ya serikali ya Rais Bashar al-Assad.
Vikosi vya serikali viliingia mjini al-Qusayr kutokea pande mbalimbali Mei 19 baada ya wiki kadhaa za mapambano na waasi, huku kukiwa na taarifa kuwa kundi la Hizbullah la nchini Lebanon limeingilia kati kuwaunga mkono wanajeshi wa serikali na vyanzo mbalimbali vinasema kuwa zaidi ya waasi 100 waliuawa katika operesheni hiyo.
0 comments:
Post a Comment